NA LAYLAT KHALFAN

MWENYEKITI wa Kamati ya Skuli ya Msingi Fuoni Mambosasa, Mohamed Simba Hassan, amekabidhi kompyuta, mipira kwa uongozi wa skuli hiyo vifaa ambavyo vilitolewa na mfanyabiashara maarufu Said Nasir Bopar.

Alisema jukumu la serikali ni kuweka miundombinu bora na kupeleka walimu wenye sifa za ufundishaji, hivyo kila mwananchi kwa nafasi yake ana fursa ya kuchangia maendeleo ya elimu, ili kiwango bora cha elimu kiweze kufikiwa.

Aidha, Simba alisema skuli hiyo inahitaji vifaa vinavyolingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa lengo la kukidhi mahitaji yanayoendana skulini hapo.

“Vifaa kama vile kompyuta, mipira, vitasaidia sana walimu na wanafunzi kujifunza kwani skuli kuna mambo mengi ya kufanywa kama vile uchapishaji wa mitihani ambayo si vizuri kuchapishwa nje kwani hupelekea kuvuja”, alisema.

Simba alisisitiza kuwa ni vyema kila mwalimu wa somo kuwa na uwezo wa kutumia komputa kwa lengo la kutunza siri kwa kazi zao.

Naye Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Abdallah Khatib Abdallah, alishukuru kwa dhati ujio wa vifaa hivyo skulini hapo kwani alidai vimekuja kwa wakati muafaka wakati vikiwa vinahitajika kwani wanafunzi watapata fursa ya kujifunza.

Aidha, alimpongeza mfanyabiashara huyo ambae pia ni mlezi wa skuli hiyo kwa kutoa msaada ambao utasaidia katika sekta ya elimu kwa kuibua vipaji vingi, hivyo aliomba wengine wenye moyo kama huo wa kujitolea kupeleka misaada kama hiyo.

Alisema licha ya kupata vifaa hivyo, lakini bado wamekabiliwa na upungufu wa vitabu vya Kiswahili, na tayari suala hilo wameshalifikisha serikalini lakini bado hawajapatiwa ufumbuzi wa hilo.

Mjumbe wa Kamati ya wazazi skulini hapo, Othman Yussuf Suleiman,alisema kwa kua wao walisoma kwa tabu enzi za ukoloni, ipo haja kwa wananchi kuthamini matunda ya mapinduzi kwa kusaidia vifaa , ili wanafunzi waweze kusoma kwa utulivu na kupata elimu yenye viwango vya hali ya juu.