NA MWAJUMA JUMA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya watoto bado inaendelea na mkakati wa kuimarisha Sauti za Watoto kupitia njia mbali mbali ikiwemo Mabaraza ya Watoto katika ngazi za Shehia, Wilaya na Taifa.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Moudline Castico, Ofisini kwake Mwanakwerekwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya Mtoto wa Kike ambayo iliyoadhimishwa jana kimataifa.

Alisema kuwa pamoja na mikakati hiyo lakini bado sauti za watoto zimezimwa na hata katika majukwaa ya umma, inayotokana na majukumu ya Kijinsia yanayobeza umuhimu wa msichana na mizizi ya mila na desturi zinazopelekea wasichana na wanawake kutothaminiwa ambayo bado yanaendeleza ukatili.

Hivyo alisema kuwa hali hiyo inachangia pia watoto hao kushindwa kupata mahitaji muhimu ikiwemo chakula, maji   na kukosa haki ya kusoma. 

Hivyo alisema kuwa wizara yake kwa kushirikiana na mashirika ya C-Sema na UNFPA wameandaa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Duniani wakiwa wanaungana na mataifa mengine duniani ambayo ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa watoto wa kike katika kuwawezesha kutatua changamoto wanazokabiliana nazo kila siku.

Alifahamisha kwamba katika siku hiyo ujumbe wa mwaka huu ni “Sauti Yangu ni Usawa wa Baadae” ujumbe ambao unatoa fursa kwa jamii na taasisi zinazoshughulikia masuala ya watoto kuzingatia sauti za Watoto wa Kike kwa kuwasikiliza na kutekeleza yale yanayowasibu watoto wa kike ikiwemo maoni yao, ushauri, matumaini yao, mipango na vipaumbele vyao katika kufikia malengo yao.

Castico alisema kuwa kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatajikita katika kuzungumza na wasichana na namna gani wadau na serikali wanaweza kutumia nafasi zao kuleta usawa wa Kijinsia katika Jamii zao.

Kwa upande wake Meneja wa Huduma ya Simu kwa Mtoto Fatma Ahmad C-Sema alisema kuwa wamekuwa na miradi mbali mbali ambayo wanafanya ili kuwalinda watoto wote ikiwemo huduma ya simu kwa mtoto ambayo katika uwepo wake wamegunduwa kwamba watoto wa kike ni wahanga zaidi katika masuala ya udhalilishaji wa kijinsia.