LONDON, England

KOCHA Mkuu wa Manchester United, Ole Gunner Solskjaer amesema kichapo cha mabao 6-1 alichopokea kutoka kwa Tottenham Hotspur ni cha udhalilishaji na kimemkasirisha.

Usiku wa kuamkia jana, Manchester United ikiwa Uwanja wa Old Trafford ilishuhuhudia ikiyeyusha pointi tatu jumlajumla mbele ya kikosi cha Jose Mourinho ambaye aliwahi kuifundisha pia timu hiyo.

Nyota wao Bruno Fernandes alipachika bao la mapema dakika ya pili kwa mkwaju wa penalti lilisawazishwa na Tanguy Ndombele dakika ya 4 na mvua ya mabao iliendelea dakika ya 7 na 37 kupitia kwa Song Heung-min na Harry Kane, ambaye pia alitupia mawili dakika ya 30 na huku lile alilopachika dakika ya  79 lilikuwa ni kwa penalti, Serge Aurier alipachika moja dakika ya 51.

United ilimaliza mchezo ikiwa pungufu baada ya Anthony Martial kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 28 jambo lililoongeza ugumu kwa Manchester United kupenya ngome ya Spurs.

Solskjaer amesema:-“Ni matokeo mabaya sana kwa timu na nimeumia sana kuona tumepoteza,kwa maana nyingine ninasema hii ni siku mbaya kwangu nikiwa kocha wa Manchester United pamoja na wachezaji pia.”