TAIPEI, TAIWAN

RAIS wa Taiwan Tsai Ing-wen amekutana na mwakilishi wa Somaliland, Mohamed Omar Hagi Mohamoud katika ikulu ya mjini Taipei ambapo viongozi hao walijadili kwa kina kuendeleza mashirikiano na mahusiano baina ya nchi hizo.

Katika mkutano huo rais Tsai alisema kukutana na mwakilishi huyo wa Somaliland kunaonesha jinsi gani mataifa hayo yalivyo na shauku kubwa ya kuongeza shirikiano katika sekta mbalimbali.

Rais Tsai alisema vyombo vya habari nchini Taiwan vimekuwa vikiripoti kwa kueleza kuwa nchi ya Somaliland ni rafiki mpya wa Taiwan, jambo ambalo alisema kuwa halina shaka yoyote.

“Vyombo vya habari huripoti kwamba Somaliland ni rafiki mpya wa Taiwan, kwa hakika ujio wako hapa ofisini umethibitisha hilo”, alisema rais huo.

Aidha alisema hatua ya Somaliland kufungua ofisi ya ubalozi nchini Taiwan inaongeza ushirikiano kwa faida ya mataifa na wananchi wa nchi hizo.

Kwa upande wake, mwakilishi huyo wa Somaliland, Mohamed Omar Hagi Mohamoud alisema amejawa na furaha sana kwani Taiwan ni nchi yenye upendo na rafiki wa kweli wa Somaliland.

Alisema taifa hilo kwa sasa linajiimarisha na kujenga misingi ya kidemokrasia ambapo pia limepokea wakimbizi kutoka mataifa kadhaa yenye machafuko kama Somalia, Yemen, Syria nan chi nyengine.

Alisema nchi yake itashirikiana na jumuiya ya kiamtaifa katika kuhakikisha inapambana na usafirishaji haramu wa watu pamoja na silaha.