NA ZAINAB ATUPAE

MASHABIKI, wadau na wapenzi wa timu ya timu ya soka ya Strong Fire ya Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini, Unguja, wamekumbushwa kuwa timu  yao, imerudi  na hivi sasa inacheza  ligi tangu msimu uliomalizika wa  mwaka 2019-2020.

Timu hiyo iliuza daraja kwa timu ya Mchangani ya Mjini ikiwa daraja la kwanza ya Unguja mwaka 2018, ambapo kwa sasa inashiriki ligi daraja la pili wilaya ya Kati.

Akizungumza na gazeti hili huko Kilimani Meneja wa timu hiyo Mwinyi Khalid Mohamed, alisema wameamua  kuichukuwa timu ya Unguja Ukuu FC na kuipa jina la timu ya Strong Fire.

Alisema sababu ya kurudishwa timu hiyo ni baada ya wazee pamoja na wazawa wa kijiji hicho, kutaka timu yao irejeshwa na ipewa jina lake la asili.

“Wazee pamoja na mashabiki walikuwa tayari kutoa pesa ili tuwalipe timu ya Mchangani na kuturejesha daraja letu,lakini tulichokifanya  kama uongozi tulichukuwa timu yetu ya Unguja Ukuu FC na kuipa jina la Strong Fire,”alisema.

Alisema sababu zilizopelekea kuuzwa timu hiyo ni baada ya mtafaruku uliojitokeza kati ya aliekuwa katibu  wa timu hiyo, kutaka kuiuza timu hiyo kwa  Dulla Boys kwa madai ya kuwa alishindwa kuongoza.

Alisema uongozi wa klabu ya Strong Fire haukuwa tayari kuona timu yao inauzwa kwa timu hiyo,lakini baada  ya changamoto kuwa kubwa walilazimika  kuiuza kwa timu ya Mchangini ya Mjini.

Aidha alisema malengo yao msimu unaokuja ni kuipandisha daraja timu yao kutoka la pili wilaya ya Kati na  kwenda Mkoa.