KHARTOUM,SUDAN

SERIKALI ya Sudan imetangaza kuwa inajadiliana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) mapendekezo matatu kuhusu jinsi ya kumfungulia mashitaka rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir, na wenzake kadhaa kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita katika jimbo la Darfur.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Sheria wa Sudan, Nasruddin Abdul Bari, baada ya mazungumzo yake na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya ICC, Fatou Bensouda mjini Khartoum.

Abdul Bari alisisitiza kuwa Sudan iko tayari kushirikiana na mahakama hiyo kwa mujibu wa sheria za kimataifa zinazoshughulikia wahalifu.

Aliongeza kuwa Sudan ilitoa mapendekezo matatu kuhusu kesi ya al Bashir na wenzake ambayo ni ama kuanzishwa mahakama maalumu, kufunguliwa mahakama mseto inayoshirikisha serikali ya Khartoum na ICC, au kupelekwa watuhumiwa hao katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai huko The Hague nchini Uholanzi.

Waziri wa Sheria wa Sudan alisema kuwa pande hizo mbili bado zinajadili mapendekezo hayo.

Kwa upande wake Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC,Fatou Bensouda alipongeza mazungumzo ya ujumbe wa mahakama hiyo na Serikali ya Sudan bila ya kutoa maelezo zaidi.

Bensouda anajaribu kuwashawishi viongozi wa Sudan waafiki suala la kukabidhiwa al Bashir na maofisa wengine kadhaa wa zamani wa nchi hiyo ili wahukumiwe katika mahakama ya kimataifa ya ICC.