MWAKA 1860, Robert Burke na William Wills walifahamika kwa kuongoza msafara wa kwanza barani ulaya ambao ulijulikana Australia yote.
Msafara huo haukwenda vizuri kutokana na uongozi mbaya na mipango isiyokuwa na utaratibu pamoja na mikosi mingi ya safari
Wakati wa kurudi, wasafiri hao walipata changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa chakula pamoja na kutokuwa na maji ya kutosha.
Hali hiyo ya kukwama jangwani bila chakula iliwapelekea kutengeneza chakula ambacho walijua ni sumu inayoweza kudhuru maisha yao, lakini walikuwa hawana njia nyingine ya kuendelea kuishi.
“Ngamia wote tuliokuwa nao walikufa kwa sababu tulikuwa hatuna chakula cha kuwapa, hali ilikuwa ngumu lakini wanakijiji wa eneo hilo la Yandruwandha walikuwa wanaishi licha ya hali ya eneo hilo”.
Walipopita katika eneo la kijiji hicho wakati wakirudi katika msafara wao, wenyeji waliwapa keki ambazo zimetengenezwa na unga wa muhogo.
Njaa za wasafiri hao Burke, Wills na King ziliwafanya kutokua na jinsi zaidi ya kula keki hizo kwa sababu walikuwa wameishiwa nguvu mwilini kutokana na kutokuwa na chakula.

Chakula kilichowafanya kupona jangwani, kilifanya watu wafanye udadisi. Chakula hicho hicho cha muhogo, mtu hawezi kusema kuwa ni sumu katika nchi nyingi za Afrika.
Wakulima barani Afrika wanalima zao hilo kwa ajili ya chakula na biashara. Ingawa hata baadhi ya maeneo nchini Tanzania baadhi ya makabila huwa ni mwiko kwao kula muhogo kwa madai kuwa una sumu.
Kwa mfano nchini Tanzania, baadhi ya wenyeji katika mkoa wa Kilimanjaro hasa kabila la wachaga wanadai kuwa chakula hicho ni sumu na hivyo kuwa na utamaduni wa kutokula mihogo.
Lakini siku za hivi karibuni hali imeanza kubadilika pia. “Sisi wachaga wa mjini hapa Dar es Salaam ndio tunakula mihogo, lakini asili yetu tangu enzi na enzi huwa hatuli mihogo kwetu kwa sababu tunaamini kuwa ni sumu.” Mtanzania mmoja mwenye asili ya uchaga alieleza.
Mihogo ni chakula ambacho kina virutubisho vingi kwa afya ya binadamu kama vitamini na madini. Kuna mihogo ambayo ni mitamu na ambayo michungu.
Utofauti wa muhogo wenye sumu na usio kuwa na sumu hutegemea eneo ambalo zao hilo umekuzwa.
Mihogo inaliwa kama chakula katika nchi zinazoendelea peke yake. Tangu mwaka 1984, zao hilo limekuwa kwa kasi barani Afrika tofauti na mabara mengine.
Bei ya mihogo katika soko la kimataifa limekuwa kutokana na ongezeko la uhitaji na bidhaa ambazo zinaweza kutengenezwa kutokana na zao hilo.
Huku wengine wakiamini kuwa mihogo kuwa dawa vilevile. Mfano jijini Dar es Salaam, mihogo imekuwa ikiuzwa mibichi barabarani.
Nchi 39 za Afrika zinalima zao hili la kuanzia Madagascar, Senegal na asilimia 70 ya maeneo ya Nigeria, DRC na Tanzania. Nchi nyingine za Afrika zinazolima mihogo kwa wingi ni Msumbiji, Uganda, Ghana, Angola na Cameroon.
Nchi hizo zinazalisha mihogo kama chakula na wanajipatia kipato kwa kilimo hicho kwa miezi 12 mpaka 24. Zaidi ya asilimia 50 ya mihogo inapatikana barani Afrika.
Je ni kweli muhogo una sumu na kuna namna ya kuondosha sumu iliyomo katika chakula hicho kinachotumiwa sana hapa Zanzibar.
Mwaka 1981, mjini Nampula, Hans Rosling kutoka nchini Sweden alisema kuwa watu wengi walifika hospitalini kwa ajili ya matibabu kwa sababu walikuwa wamepooza.
Ilidaiwa kuwa ni ugonjwa wa polio ingawa dalili zake hazikuwahi kuandikwa katika kitabu lakini sababu za kuugua kwao kulitokana na kula mihogo.
Barani Afrika…mihogo ilianza kuliwa katika karne ya 17 mara baada ya watu kuelewa kanuni za ulimaji wake.
Muhogo ni chanzo cha tatu cha chakula baada ya mchele na mahindi barani Africa. Na sasa chakula hichi kimejipatia umaarufu mkubwa mno baada ya kuhusishwa na faida kabambe kwa jinsi ya kiume.
Lakini wengi sijui kama tunajua kuwa muhogo una sumu aina ya ‘cyanide’ ambayo inaweza kusababisha hata kifo kwa binaadamu anayekula chakula hicho.
Muhogo una kemikali zinazoitwa ‘cyanogenic glycosides’ ambazo zinaweza kutoa kemikali ya ‘cyanide’ ambayo ni hatari inapotumiwa na mwanadamu. Inapoliwa mara kwa mara, kemikali hizi zinaongeza hatari ya sumu ya ‘cyanide’, ambayo inaweza kuathiri utendakazi wa viungo kama tezi (thyroid) na mfumo wa neva.
Aidha, ‘cynanide’ inahusishwa pakubwa na ulemavu na kudorora kwa viungo, jambo linaloweza kusababisha kifo. Watu walio na utapia mlo na wanaokula protini kidogo ndio walio katika hatari kubwa zaidi ya kupatwa na tatizo hili.
Kwa sababu sumu hii inayotokana na ‘cyanide’ ni jambo linalojadiliwa sana haswa na wanaoishi katika mataifa yanayoendelea.
Baadhi ya njia unazoweza kutumia kuhakikisha muhogo ni salama kwa kuliwa ni pamoja na kuutoa maganda ambayo ndiyo yenye kiwango kikubwa cha kemikali zinazosababisha sumu ya cyanide.

Pia unatakiwa uroweke, kwa maji kwa muda wa saa 48-60 kabla ya kuupika, kwani kwa kufanya hivyo kunawezesha kuondoka kwa sumu zilizomo katika muhogo.
Kwa kuwa kemikali hatari zinapatikana ndani ya muhogo, ni muhimu kuupika kwa umakinifu ikiwa ni kwa kuuchemsha, kuuchoma au kwa kuoka, pia unaweza kuuambatanisha kwa kuupika na chakula chengine.
Wataalamu wanashauri kuuambatanisha muhogo kwa kuupika kwa kuuchanganya na vyakula vyenye protini kuna faida hasa ikizingatiwa kuwa protini husaidia kuondoa cyanide mwilini.
Kwa wale wanaopenda kula muhogo lazima waelewe kuwa unapokula mbichi jua kuwa unachukua kiwango kikubwa cha sumu na kadiri utakavyokua mchungu ndio kadiri ya kiwango kikubwa cha sumu.