TOKYO,JAPAN

KAMPUNI ya kutengeneza magari ya Suzuki Motor ya Japani inasema imetengeneza kifaa kinachowezesha mota za nje ya boti kukusanya taka ndogo za plastiki zinazoweza kuwa tishio kwa mifumo ikolojia.

Suzuki ilikuwa ikifanya tafiti kwa miaka mingi ikijaribu kushughulikia uchafuzi wa maji unaosababishwa na taka za plastiki.

Kampuni hiyo inasema ililenga mota za nje ya boti zinazosukuma tani nyingi za maji ya kupoozea.

Kifaa hicho kimewekwa kwenye tundu la maji yanayorejea na kinachuja uchafu ulio kwenye maji hayo.

Kampuni hiyo inasema taka ndogo ya plastiki iliyo karibu na nyuso za maji inaweza kukusanywa kwa kuiendesha  boti hiyo.

Wafanyakazi wa kampuni ya Suzuki walifanya majaribio kwenye Ziwa Hamana mkoani Shizuoka.

Kifaa hicho kilikusanya mwani,mchanga na vitu vyengine vikiwemo vipande vidogo vinavyoonekana kuwa plastiki.

Kampuni ya Suzuki inasema inataka kukiweka kifaa hicho sokoni ndani ya mwaka ujao.