NA MWANDISHI WETU

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tamwa Zanzibar kwa kushirikiana na shirika la Action Aid kwa lengo la kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, wamewapatia mafunzo wanajamii 660 kutoka shehia 22 wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Ofisa anayeshughulikia maswala ya udhalilishaji kutoka TAMWA-Zanzibar, Zaina Salum Abdalla alisema lengo la mafunzo hayo kwa wanajamii hususani wanawake ni kujengewa ufahamu zaidi juu ya dhana nzima ya udhalilishaji na madhara yake.

Alieleza kuwa anaamini elimu iliyotolewa kwa muda wa wiki mbili kwa wanajamii italeta mabadiliko kwa wanajamii kupambana na aina mbalimbali za udhalilishaji sambamba na kuviripoti vitendo hivyo katika vyombo vya sheria.

Alisema kuwa katika maeneo ya hapa Zanzibar wapo baadhi ya wanajamii huyafumbia macho matendo hayo kwa wanawake na watoto kutokana na   sababu mbali mbali ikiwemo hofu ya kuvunjika kwa ndoa zao.

‘’Kuna matukio ya udhalilishaji yanafanyika lakini watu wapo tayari kuona yanaendelea, lakini hushindwa kusema kwa kuhofia kupewa talaka na waume zao’’, aliongezea.

Hata hivyo, ofisa huyo aliiasa jamii kubadilika na kutokuwa na muhali badala yake watoe taarifa dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuchukuliwa hatua kwa watendaji watakaobainika.

Akizungumza kwa niaba ya masheha, sheha wa Kitope Khamis Ndende Juma alisema wanakabiliwa na matukio ya udhalilishaji kwenye jamii zao kiasi cha kwamba walio wengi wameanza kushtuka na kuhofia madhara zaidi.

Alisema suala la muhali bado ni tatizo ambalo wanaendelea kukabiliana nalo ndani ya jamii zao kwa kuwa wapo baadhi ya watu wanatendewa matendo hayo na kisha kuamua kunyamaza kimya.

Mzee Ali Makame kutoka shehia ya Kitope alisema ili jamii iweze kumaliza tatizo hilo ipo haja kuhakikisha wazazi na walezi wanakua karibu zaidi na watoto wao kila wakati.

Kwa upade wake ofisa Dawati la Jinsia Mkoa wa kaskazini Unguja Salum Khamis Machano alisema jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana na matukio hayo ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote wanaofikishwa katika dawati hilo.

Hata hivyo ofisa huyo alisema bado kuna tatizo ndani ya jamii ikiwemo la kukosa utayari wa kuendelea na baadhi ya kesi ambazo huwa tayari zimeshafikishwa katika vituo mbali mbali vya polisi.