NA GASPARY CHARLES

WANAVIKUNDI vya ujasiriamali kisiwani hapa wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa mitandao ya kijamii kuongeza wigo wa kutangaza na kuuza bidhaa zao kupitia soko mtandao.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi hivyo juu ya matumizi ya soko mtandao yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA Zanzibar) Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Faki Othman Faki, alisema ili mjasiriamali aweze kukua kiuchumi ni lazima ajue kutumia fursa ya mitandao ya kijamii.

Alisema uwepo wa mitandao hiyo imerahisisha uwezekano wa mjasiriamali kuuza na kuwafikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi pasipo kutumia nguvu.

“Ni muhimu kuchangamkia fursa ya soko mtandao kwani ndiyo sehemu pekee kwa sasa ambayo inaweza kukutanisha na wateja wengi zaidi na kwa haraka duniani pasipo kutumia nguvu nyingi,” alisema.

Aidha mwezeshaji huyo alitahadharisha wajasiriamali hao kuachana na dhana ya kuzalisha bidhaa kwa mazoea kwani kufanya hivyo kutapelekea kuwakosesha wateja kutokana na bidhaa hizo kukosa mvuto.

Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia misingi ya masoko ikiwa ni pamoja na kimarisha mahusiano na mawasiliano chanya kwa wateja ili kujenga uaminifu kwa wateja  wa bidhaa zao.

Mmoja wa washiriki, Fadhila Ali Juma alishukuru kutolewa kwa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa soko kwa bidhaa zao.