Na Gaspary Charles

WANAVIKUNDI vya ujasiriamali kisiwani Pemba wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa mitandao ya kijamii kwaajili ya kuongeza wigo wa kutangaza na kuuza bidhaa zao kupitia soko mtandao.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi hivyo juu ya matumizi ya soko mtandao yaliyoandali wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar mwezeshaji wa mafunzo hayo, Faki Othman Faki amesema ili mjasiriamali aweze kukua kiuchumi ni lazima ajue kutumia fursa ya mitandao ya kijamii.

Alisema uwepo wa mitandao hiyo imerahisisha uwezekano wa mjasiriamali kuuza na kuwafikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi pasipo kutumia nguvu kubwa kama ilivyo kwa njia nyingine za utaftaji wa masoko.

“Ni muhimu sana kuchangamkia fursa ya soko mtandao kwani ndiyo sehemu pekee kwa sasa ambayo inaweza kukutanisha na wateja wengi zaidi na kwa haraka duniani pasipo kutumia nguvu nyingi,” alisema.

Aidha mwezeshaji huyo alitahadharisha wajasiriamali hao kuachana na dhana ya kuzalisha bidhaa kwa mazoea kwani kufanya hivyo kutapelekea kuwakosesha wateja kutokana na bidhaa hizo kukosa mvuto na ubora wa kushindana na bidhaa nyingine sokoni.

Pia aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia misingi ya masoko ikiwa ni pamoja na kimarisha mahusiano na mawasiliano chanya kwa wateja ili kujenga uaminifu wa wateja kwa bidhaa zao.

Alisema, “tuache taba ya kuzalisha bidhaa kwa mazoea na badala yake tujenge misingi ya kuwa na mawasiliano ya karibu na wateja wetu ili kujua mahitaji yao kwani hii itakusaidia kujua wapi panahitaji kuboreshwa ili kuendelea kuaminika zaidi sokoni.”

Mmoja wa washiriki hao, Fadhila Ali Juma ameshukuru kutolewa kwa mafunzo hayo kwani itawasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa soko kwa bidhaa walizokuwa wanazalisha.

“Kiukweli leo nimefurahi sana kupata mafunzo haya kwani kuanzia leo kikundi chetu tutaanza kutumia fursa hii tuliyooneshwa kwaajili ya kuuza bidhaa zetu ambazo ni, Sabuni asilia, Mafuta na majani ya chai kwani changamoto kubwa inayotukabili ni upatikanaji wa masoko tunazalisha sana lakini soko ni kikwazo,” alisema.

Mapema afisa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar – (WEZA III) kutoka TAMWA ofisi ya Pemba, Asha Mussa Omar alisema lengo la kutolewa mafunzo hayo ni kuwapatia mbinu za kuongeza wigo wa upatikanaji wa soko la kuuza bidhaa zao wanazozalisha ili lengo la kujikwamua kiuchumi lifanikiwe.