NA KIJA ELIAS, MOSHI

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA, limesema limeendelea kuchukua tahadhari zote, kuhakikisha kwamba moto uliozuka hapo jana hauta athiri kwa kiwango chochote kile shughuli za nzima za upandaji mlima.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mawasiliano wa TANAPA, Pascal Shelutete, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema shirika hilo, limeendelea kuchukua tahadhari zote, ili kuhakikisha kwamba usalama wa wageni na vifaa vyote unaimarishwa bila kuathiri shughuli zozote za utalii ambazo zinaendelea katika mlima huo.

“Shirtika la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA limechukua tahadhari zote katika kuhakikisha kwamba moto huu uliozuka hapo jana hauta athiri shughuli zozote za upandaji mlima,”alisema.

Shelutete alisema kuwa moto huo, ulianza kuwaka jana majira ya jioni katika eneo la Whona  ambapo ni kituo cha kupumzikia wageni wanaotumia njia ya Mandara  na Horombo na kwamba unaendelea kudhibitiwa  kwa kushirikiana na wananchi wanaozunguka hifadhi ya mlima huo pamoja na vikosi vinavyoshiriki zoezi hilo la uzimaji moto.

Aliongeza kusema kuwa “Moto huo uliozuka jana katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro KINAPA, katika eneo la Whona kwenye kituo cha kupumzikia wageni  wanaotumia  njia ya Mandara na Horombo, lakini hadi sasa unaendelea kudhibitiwa na vikosi  vinavyoshiriki zoezi hilo,”alisema Kamishna Msaidizi Mwandamizi  Mawasiliano.

Alisema kuwa “Matumaini yapo kwamba moto huu utaweza kuudhibiti kwa kadri ya nguvu kazi ambayo tunazo, jitihada zinafanyika za kutosha na moto huu utaweza kuudhibiti katika muda si mrefu,”alisema.

“Kama ambavyo manafahamu Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro KINAPA ni maarufu sana kwa kupokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi ambao hufika kwa ajili ya shughuli za utalii hususan kupanda mlima huo”alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Usimamizi Wanyama Pori (Mweka), Profesa. Jafari Kadegesho, alisema baada ya kupata taarifa za kuungua kwa mlima huo hivyo kama wadau wakuu tumeona ni muhimu  wafanyakazi na wanafunzi wetu kwenda mlimani kushiriki  kuzima moto huo.