RABAT,MOROCCO

MAOFISA  wa Serikali ya Morocco wametangaza kuwa wamefanikiwa kukamata tani 5.6 za bangi katika operesheni mbili tofauti zilizofanyika nchini humo.

Shirika rasmi la habari la Morocco MAP limetangaza habari hiyo na kuwanukuu maofisa wa Serikali wakisema kuwa, askari wa Kikosi cha Gadi ya Fukwe cha Morocco, walifanya doria katika ufukwe wa kilomita nne magharibi mwa mji wa al Hoceima wa kaskazini mwa nchi hiyo na kukamata mafurushi 117 ya bangi yenye uzito wa tani nne.

Madawa hayo ya kulevya yalikuwa yamefichwa kwenye mtaro karibu na ufukwe wa Inouaren yakisubiri kusafirishwa kimagendo kwa njia ya baharini. 

Katika opereseheni ya pili, maofisa wa kulinda usalama katika mji wa Guelmim wa katikati mwao Morocco walifanikiwa kukamata bangi yenye uzito wa tani moja na kilogramu 630.

Madawa hayo haramu yalikuwa yamefukiwa jangwani karibu na eneo lisilo la hema lisilokaliwa na watu.

Inaonekana kuwa hema hilo lilijengwa kama alama ya kujua wahalifu walipofukia bangi hiyo.

Maofisa usalama wa Morocco wanasema uchunguzi unaendelea kuwagundua wahalifu waliokuwa wamefukia bangi hiyo kwenye eneo hilo.

Mbali na juhudi mbalimbali za kupambana na upandaji wa bangi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, lakini Morocco inaendelea kuwa mzalishaji mkubwa wa bangi duniani.

Hayo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Uhalifu na Mihadarati.

Vyombo rasmi vya Morocco vilisema kuwa mwaka 2019, maofisa usalama wa nchi hyo walikamata tani laki moja na 79 elfu na 657 za bangi.