NA BEATRICE SANGA, MAELEZO

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetia saini mikataba miwili ya msaada kati yake na Serikali ya Uswisi,ambapo katika mikataba hiyo miwili, Serikali ya Uswisi imetoa msaada wa Faranga za Uswisi Milioni 15.75, sawa   na Shilingi za Tanzania Bilioni 39.59.

Msaada huo unalenga kusaidia jitihada za Tanzania kufikia malengo ya kusaidia Sekta ya Afya kwa wote na kupunguza malaria nchini.

Hafla hiyo, imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mount Meru uliopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James, ameeleza kuwa, Tanzania imesaini mikataba miwili ambapo mkataba wa kwanza ni msaada wa Faranga za Uswisi Milioni 9.75, sawa na Shilingi Bilioni 24.51 za kitanzania ambazo zimetolewa ili kugharamia mradi wa uboreshaji wa afya na uimarishaji wa mfumo wa afya (HPSS).

Mkataba wa pili ni wa msaada wa Faranga za Uswisi Milioni 6, sawa na fedha za kitanzania Shilingi Bilioni 15.08 zilizotolewa kwa ajili ya kugharamia programu ya kutokomeza malaria nchini Tanzania ambapo kwa mwezi Oktoba 2020 pekee Tanzania imeweza kusaini mikataba ya jumla ya pesa za kitanzania Bilioni 83.69.

“Wakati tunasaini mikataba hii leo, pia ikumbukwe kuwa tarehe 6 Oktoba, 2020 Serikali zetu mbili zilisaini mikataba miwili ya misaada yenye thamani ya Faranga za Uswisi Milioni 17.80, sawa na Shilingi Bilioni 44.10. Kwa hiyo, kwa mwezi Oktoba 2020 pekee tumesaini mikataba ya misaada ya jumla ya Faranga za Uswisi Milioni 33.55 sawa na Shilingi Bilioni 83.69.” Amesema Doto James.

Doto James, ameongeza kuwa pesa hizo zitaenda kutumika kuimarisha Mifumo ya Afya hapa Tanzania kwa kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF) wenye malengo mahususi ya kuimarisha Sekta ya Afya.

Aidha ameongeza kuwa, Faranga za Uswisi Milioni 6 sawa na Shilingi Bilioni 15.08 zilizotolewa kwa ajili ya Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania zitaenda kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na maralia pamoja na kutekeleza mikakati ya kisekta ya kuzuia maambukizi mapya ya Malaria.

“Tutaweka Mpango wa Kudhibiti Malaria Tanzania kwa lengo la kuondoa kabisa vifo vinavyotokana na malaria na kupanua wigo wa maeneo yasiyokuwa na malaria (Malaria Free Zones) hadi nusu ya nchi nzima ifikapo mwaka 2030 kupitia utambuzi wa maeneo hatarishi kwa Malaria nchini” amesema Doto James.