NA AHMED MAHMOUD, ARUSHA
WAKALA  wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) Mkoani hapa, umeeleza kusikitishwa na baadhi ya wananchi wanaohujumu miundombinu ya barabara kwa kuiba kingo za madaraja na  vyuma vilivyowekwa alama za barabarani na kuviuza mali chakavu.

Mratibu wa TARURA, Mkoa wa Arusha, Mhandisi Edward Amboka,  aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo na kuwataka wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja.

‘’Hali hii licha ya kusababisha hasara na kutumia gharama kubwa kuvirejesha pia imekuwa ikichangia madereva kuvunja sheria za usalama barabarani kutokana na kutokuwepo kwa alama hizo, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likichangia ajali za mara kwa mara”alisema

Mhandisi Amboka, aliiomba Serikali kufanye ukaguzi wa kushitukiza wa mara kwa mara katika maeneo yote ya mkoa wa Arusha, ambapo hufanyika biashara ya vyuma chakavu na kuwakamata wale watakaobainika kukutwa na
vyuma hivyo vya barabarani, ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Pia niwaombe wananchi wawe walinzi wa miundombinu hii kwani iko kwa ajili yao kwa kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo hivi na pia niwaombe wananchi kuacha kuwaga takataka katika mitaro ya barabara
kwani inachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa barabara”alisisitiza.