HABIBA ZARALI

MKUU wa Kitengo cha Taaluma, Kifua Kikuu, Ukoma, Homa ya Ini na Ukimwi Hasnuu Fakih Hassan, amesema dhana potofu ikiwemo ya uchawi ni jambo moja linalorejesha nyuma juhudi za mapambano ya ugonjwa wa Kifua Kikuu.


Alisema wananchi wengi wanapokuwa na dalili za ugonjwa wa TB, huamua kukimbilia kwa waganga wa kinyeji jambo ambalo sio sahihi kwani huchangia kuongezeka kwa ugonjwa huo.

Mkuu uyo wa kitengo alisema ni vyema kwa  wananchi  kuwa na utamaduni wa kukimbilia hospitali kufanya kipimo cha  kifua kikuu mara tu wanapogundua dalili zake kwa lengo la kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.

Alisema kukohoa, homa kali hasa wakati wa usiku, uchovu ni miongoni mwa dalili za TB hivyo zinapojitokeza ni vyema kukimbilia hospitali mapema.


Wakati huohuo,  alizitaka familia zenye wagonjwa wa TB ambao tayari wameanza kutumia dawa kuwasimamia, ili kutumia kwa mpango kwani kutofanya hivyo kunaweza kuleta matatizo.

Nao baadhi ya  wagonjwa waliofika hospitalini hapo kupata matibabu walisema ugonjwa huo unatisha mtu anapousikia lakini mgonjwa akitumia dawa  kwa usahihi unapona haraka