BANGKOK, THAILAND

SERIKALI nchini Thailand imetangaza hali ya dharura kwa lengo la kumaliza maandamano yanayoongozwa na wanafunzi, ambayo yamedumu kwa miezi mitatu yanayotaka marekebisho kwa ufalme na kujiuzulu kwa waziri mkuu Prayuth Chan-ocha.

Polisi wamewatawanya waandamanaji walioweka kambi nje ya ofisi ya waziri mkuu wa nchi hiyo, baada ya amri mpya ya kuzuia mikusanyiko kuanza kutekelezwa kote nchini humo.

Muda mfupi tangu kuanza kutekelezwa kwa amri hiyo, polisi wa kutuliza ghasia waliwatawanya waandamanaji hao, ambao baadhi yao walijaribu kuweka vizuizi kwa kutumia chupa na makopo.

Polisi hao pia walifanya doria katika baadhi ya mitaa ya Bangkok, huku wanasheria wa haki za biandamu wakisema viongozi watatu wa maandamano hayo wamekamatwa.

Mfululizo wa maandamano ya umma yanayoendelea kwa miezi mitatu sasa, umevutia maelfu ya watu katika mitaa ya mji mkuu wa Bangkok kushindikiza kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Prayuth Chanocha na kuandikwa kwa katiba mpya ya Thailand.

Uamuzi huo unapiga marufuku mikutano ya watu watano au zaidi na uchapishaji wa habari au ujumbe kwenye mitandao, ambao unaweza kudhuru usalama wa kitaifa.

Televisheni ya serikali ilisema, “Ni muhimu kuanzisha hatua ya haraka kumaliza hali hio kwa ufanisi ili kudumisha amani na utulivu”.