NA MWANDISHI WETU

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB) imewataka wananchi kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi ili kuhifadhi amani wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

Mwenyekiti wa  tume hiyo Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu, alieleza hayo katika taarifa kwa vyombo vya habari na kuwahimiza Watanzania waliotimiza vigezo kwa mujibu wa sheria, kujitokeza kwenda kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu huku mamlaka nyengine zikitimiza wajibu wake kikamilifu.

“Tume, inapenda kuchukua fursa hii kuzipongeza Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kulipa uzito tukio hilo na kutoa fedha za kuligharamia ili wananchi waweze kutimiziwa haki yao ya kikatiba,” alisema jaji mwaimu katika taarifa hiyo.

Aidha alizipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa maandalizi mazuri na mwendelezo wa utoaji elimu ya uraia kwa wananchi kuhusu uchaguzi mkuu na kuziomba kusimamia hatua za  mchakato wa uchaguzi kwa weledi, sheria na kanuni za nchi.

“Pia Tume inalipongeza Jeshi la Polisi kwa kulinda usalama wa raia na mali zao katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi. Vilevile, vyombo vya habari kwa kuzingatia haki ya kikatiba ya wananchi kwa kuwahabarisha kuhusu matukio na sera zilizokuwa zinanadiwa na wagombea na vyama vyao,” alisema Mwenyekiti huyo.

Jaji mwaimu alieleza kuwa katika kipindi kilichobakia kufikia siku ya uchaguzi, alilitaka jeshi la polisi kusimamia amani ili wananchi watimize haki yao ya kidemokrasia na wanapotekeleza majukumu yao kutotumia nguvu.

“Tuanaliomba Jeshi la Polisi kulinda amani na usalama wa wananchi wanapotekeleza majukumu yao wazingatie maadili, waheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora pamoja na kuepuka matumizi makubwa ya nguvu yasiyokuwa ya lazima,” alisema.

Kwa upande wa mamlaka zenye dhamana ya kusimamia uchaguzi, mwenyekiti huyo alizitaka zihakikishe uchaguzi mkuu unasimamiwa kwa haki na amani wakati wote sambamba na kuhakikisha wanadumisha amani wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa wazi, wenye amani na utulivu.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaohusisha uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani utafanyika leo huku watendaji wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama waliopo katika majukumu ya uchaguzi wakiruhusiwa kupiga kura mapema.