NAIROBI, Kenya

OFISA mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Barry Otieno ameonya kwamba klabu za Kenya, zinaweza kujikuta zikikosa mechi za kimataifa barani Afrika msimu ujao kama ligi kuu ya Kenya haitaanza hadi mwezi ujao.

FKF tayari imetoa ratiba ya mechi za Ligi Kuu kwa minajili ya muhula ujao wa 2020-21 ambapo mabingwa watetezi na washindi mara 19, Gor Mahia watashuka dimbani kuvaana na Tusker FC mnamo Novemba 21.

Hata hivyo, kuanza kwa ligi hiyo yenye timu 18 kunategemea ufanisi wa FKF kupata idhini ya serikali, ambayo imeorodhesha soka miongoni mwa michezo ya kugusana na yenye hatari zaidi katika kuchangia maambukizi ya virusi vya corona.

Soka ni miongoni mwa michezo ambayo Wizara ya Michezo iliondoa kwenye orodha ya fani kadhaa ambazo ziliidhinishwa kurejea mazoezi na mashindano ya kawaida mnamo Septemba 18.