NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wakulima wa mwani kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za msimu zinazotarajiwa kuanza Novemba mwaka huu hadi Aprili mwakani.

Pia mamlaka na wananchi nchini kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari hasi zinazoweza kujitokeza.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa utabiri wa mvua za msimu, Mkurugenzi wa mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi alisema kuwa kutokana na mvua hizo athari zinaweza kutokea kama hali ya unyevunyevu ardhini inatarajiwa kuwa ya kuridhisha kwa ajili ya kilimo na malisho katika maeneo mengi.

Alisema matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kusababisha mafuriko na kupelekea uharibifu wa miundombinu, upotevu wa maisha na maisha na mali.

Pia alisema magonjwa mengi ya milipuko yanaweza kujitokeza kutokana na kutuama kwa maji machafu na uchafuzi wa maji safi.

Dk.Kijazi alisema kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa  mikoa mingine Tabora ba Katavi.

Alisema maeneo ya mikoa ya Kigoma, Rukwa, pamoja na magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi yanatarajiwa kupata mvua za za wastani hadi chini ya wastani.

Aidha alisema vipindi vya mvua nyingi vinatarajiwa katika miezi ya Januari na Aprili  mwakani, ambapo mvua zinarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba  mwaka huu kwa maeneo ya mkoa wa Tabora, na kutawanyika katika mikoa mingine inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka katika wiki ya tatu ya mwezi Novemba mwaka huu.

Alieleza kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, na pwani ya kusini katika wiki ya nne ya mwezi Aprili mwakani na kwa mkoa wa Ruvuma mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili mwakani.

Aliongeza msimu wa vuli Oktoba hadi Disemba mwaka huu, katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua katika mikoa ya Kagera,Geita,Mwanza,Shinyanga,Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro ,pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba,unaotarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa hapo awali ambapo maeneo mengi yalitarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani.