OKTOBA 1 mwaka 2020, habari iliyoushitua ulimwengu ilihusu kuthibitishwa kwa rais wa Marekani, Donald Trump kuambukizwa virusi vya corona ikiwa ni siku chache baada ya mchuano wa kwanza wa mdahalo wa kuwania kiti cha urais dhidi ya mipinzani wake Joe Biden.

Taarifa za Trump kuambukizwa corona iliibuka saa chache baada ya mmoja kati ya wasaidizi wake wa karibu, Hope Hicks ambaye alisafiri naye hadi Cleveland kwenye mdahalo wa kuwania urais naye kubainika kuwa na virusi hivyo.

Viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani wametoa salamu za kumtakia afya njema rais huyo wakati huu akiwa amelazwa katika hospitali ya jeshi Walter Reedalidai akipatiwa matibabu ya corona.

Miongoni mwa waliomtakia afya njema ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwneguni, Dk. Tedros Adhanom Gebreyesus, mtu ambaye kwa hakika alizozana sana na Trump kuhusu virusi vya corona.

Trump alilitia msukosuko shirika hilo katika wakati ambapo dunia ilihitaji umoja katika kukabiliana na corona na hatika hali iliyokuwa haikutarajiwa alitoa shutuma kadhaa na mwishowe nchi yake kuitoa katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Trump mara kwa mara alilishutumu shirika hilo kwa kushindwa kukabiliana vyema na kusambaa kwa corona na kueleza nia yake ya kuliondolea ufadhili huku ikidai shirika hilo linaipendelea China.

Kwa hakika hatua ya rais huyo akuambukizwa virusi vya corona kumedhirisha uongo wa kiongozi huyo uliotokana na kauli zake pamoja na vitendo vyake dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa miezi kadhaa Trump alipuuza hatari za kuambukizwa ugonjwa wa corona sambamba na kuwakejeli watu wanaojaribu kujilinda kwa kuvaa barakoa, huku akiutaja ugonjwa huo kuwa umeingizwa nchini humo na chama cha upinzani cha democratic.

Pamoja na takwimu kuonesha kuwa Marekani ndio taifa lenye maambukizi makubwa ya corona na ndiyo taifa linaloongoza kwa vifo vinavyotokana na ugonjwa huo, Trump amekuwa akisema hali sio mbaya kama inavyosemwa.

Kwa mujibu wa takwimu hadi Oktoba 5 mwaka huu, watu wapatao milioni 7,636,912 nchini Marekani wameambukizwa ugonjwa huo, huku idadi ya waliofariki ikifikia 214,611 na watu 4,849,269 wakithibitishwa kupona corona.

Majaribio yote ya kuondoa nadhari kwenye kushindwa kwake, ukweli kwamba hakuna mkakati wa kitaifa wa kuwalinda raia, kwamba magavana wameachwa peke katika kupambana na ugonjwa huo.

Uhalisia umefichuka na uongo wa wote wa rais sasa hivi upo hadharani yeye pamoja na maofisa wake hawatafanikiwa tena kuwasha mishumaa ya moshi, katika kuyawasilisha maandamano ya vurugu kwenye baadhi ya miji kuwa hatari zaidi ya ukweli kwamba Wamarekani 1000 hufa kila siku kutokana na virusi hivyo.

Kwa nguvu zake zote na bila kujali hasara, Donald Trump amejaribu kuufufua uchumi kabla ya siku ya uchaguzi. Kwa tukio hili la kuambukizwa virusi, mpango huu pia umekuwa batili.

Hata wakanushaji wa corona hawataweza kuepuka kukiri kwamba virusi hivyo vina uwezo mkubwa wa kusambaa – ikiwa vimeweza kumfikia hata mtu mwenye nguvu aliyoko ikulu ya White House.

Katika kipindi hili chote cha maambukizi ya corona, Trump anadai kuwa kuwa serikali yake imekuwa na mafanikio katika kupambana na virusi hivyo.

Hata hivyo, kuugua kwake yeye, mkewe, Melania, meneja wa kampeni zake za uchaguzi Bill Stepien, washauri na wasaidizi wake ugonjwa wa COVID-19 ni kieleelzo cha kushindwa mwanasiasa huyo katika uwanja huo.

Trump ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali ya kijeshi ya Walter Reedalidai, alidai kwamba hali yake ya kiafya inaendelea vizuri na kwamba atarejea White House hivi karibuni.

Daktari Vinay Gupta ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya mapafu katika Chuo Kikuu cha Washington alisema kulikuwa na uwezekano wa Trump kuepuka ugonjwa huo.

Alisema kama kiongozi huyo kama angechukua tahadhari na kufuata maagizo yaliyotolewa ikiwemo kuacha kwenda kwenye mikusanyiko na mujumuiko isiyo na mpangilio na nidhamu asingepata ugonjwa huo.

Trump amepatwa na virusi vya corona miezi kadhaa baada ya kupuuza virusi hivyo na kutoa matamshi ya kustaajabisha na yasiyo ya kisayansi wala kielimu kuhusu virusi hivyo.

Tangu virusi vya corona vilipojitokeza na baadaye kuenea maeneo mengi ya Marekani, Trump alifanya jitihada kubwa za kudogesha hatari ya virusi hivyo na baadaye akafanya masihara na hata kutoa matamshi ya kushangaza kuhusu jinsi ya kutibu virusi hivyo.

Trump amekuwa akidai kwamba kwamba serikali yake imefanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona na hata kutengeneza chanjo yake.

Amekuwa akifanyia masihara maagizo yanayotolewa na wataalamu kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya corona kama ulazima wa kuvaa barakoa, kuchunga masafa baina ya watu katika jamii na kuosha mikono kwa sabani na vitakasa mikono mara kwa mara.

Vilevile katika mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa rais na mpinzani wake kutoka chama cha Democratic, Donald Trump alimkejeli na kumfanyia istihizai Joe Biden kwa sababu ya kuvaa kwake barakoa.

Wamarekani pamoja walimwengu wanashuhudia kwamba, kama ilivyokuwa katika masuala mengine mengi, Trump amepatwa na corona ambayo amekuwa akidai kuwa ameidhibiti na kutengeneza chanjo yake.

Trump amekuwa akikosolewa sana kutokana na uzembe na sera zake mbovu katika suala la kupambana na maambukizi ya virusi vya corona na amekemewa mara kadhaa na wataalamu wa masuala ya tiba kwa sababu ya kutoa matamshi yasiyo ya kitaalamu kuhusu virusi hivyo.

Rais huyo amekuwa mhubiri mkubwa zaidi wa habari na taarifa zisizo sahihi kuhusu maambukizi ya virusi vya corona. Kwa mfano mnamo Aprili 23 mwaka huu alidai kuwa inawezekana kutibu virusi vya corona kwa kuwadunga wagonjwa vitakasa mikono.

Hivi karibuni alidai kuwa serikali ya Marekani itakuwa imetayarisha chanjo ya corona hadi kufikia mwezi Oktoba na kwamba dozi milioni 100 zitakuwa zimetolewa hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Wataalamu wengi wa masuala ya tiba walitilia shaka madai hayo na kutangaza kuwa, chanjo na tiba ya corona haitapatikana mwaka huu.

Daktari wa Trump, Sean Conley alisema hali yake ni nzuri na anaweza kuendelea na majukumu yake akiwa karantini, hata hivyo Spika wa baraza la wawakilishi nchini Marekani, Nancy Pelosi ambaye ni mpinzani mkubwa wa kisiasa wa Donald Trump, aliwataka madaktari wanaomuhudumia rais huyo kutoa taarifa sahihi kwa wananchi dhidi ya hali ya afya ya kiongozi huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Sean P. Conley daktari wa White House alieleza kuwa iwapo mchakato wa kupata nafuu rais Donald Trump utaendelea basi anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali.

Pamoja na daktari huyo kuelezea kuendelea vyema kwa afya ya rais huyo, lakini vyombo vyengine vya habari vimenukuu vyanzo vya habari vikieleza kuwa hali ya kiongozi huyo hairidhishi.

Baadhi ya kauli za Trump kuhusu corona?  Januari 22 mwaka huu maambukizi ya kwanza ya virusi vya corona yalithibitishwa Marekani hata hivyo alisema “Tumeudhibiti kabisa. Ni mtu mmoja tu anayetokea China. Tumeudhibiti. Hali itakuwa sawa.”

Mnamo Machi 9 mwaka huu alitoa kauli akivilinganisha virusi vya corona na mafua. “Kwahiyo mwaka jana raia 37,000 wa Marekani walifariki dunia kutoka na homa. Wastani wake ni kati ya 27,000 na 70,000 kwa mwaka. Hakuna ambacho kimesitishwa, maisha na uchumi yanaendelea… Fikiria kuhusu hilo!”

Machi 31 mwaka huu alisema corona sio homa. “Sio homa. Ni ukatili. Unapompeleka rafiki yako hospitalini… inakuwa ndio kwaheri, mkakamavu, mzee kiasi, mzito kidogo kuliko alivyotaka kuwa. Na ukipiga simu siku inayofuata kuuliza, ‘anaendeleaje?’ Amepoteza fahamu? Hii sio homa.”

Aprili 3 mwaka huu akasema, “Kuvaa barakoa, litakuwa jambo la kuchagua mwenyewe. Unaweza kufanya hivyo lakini sio lazima. Mimi sitavaa, nachagua kutovaa barakoa, lakini wengine huenda wakataka kuvaa na hivyo pia ni sawa”

Julai 21 mwaka huu alisema, “Tunamtaka kila mmoja ambaye atashindwa kutekeleza hatua ya kutokaribiana, kuvaa barakoa, vaa barakoa.”

Septemba 10 alisema “Tunakaribia kukabiliana na janga, na mengine mengi mazuri yanaendelea kutokea kuhusu chanjo na tiba”.

Kuambukizwa corona Trump kumesababisha hali ya sintofahamu kuhusu mustakbali wa kisiasa wa Marekani katika masuala ya uongozi wa nchi hiyo, zeoezi la uchaguzi, midahalo ya kisiasa na hata uchaguzi wenyewe, na suala hilo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani.