MWISHONI mwa mwezi Septemba gazeti la New York Times limelipua bomu na kufichua kwamba rais Donald Trump alilipa kiasi cha dola 750 tu za kodi ya mapato.

Trump amefanya kazi kwa miongo kadhaa akijenga taswira yake kama mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na hata kuchagua kujipachika jina la tajiri kigogo.

Gazeti hilo lilifichua kwamba alilipa kiasi cha dola 750 katika kodi ya mapato katika mwaka 2016, mwaka ambao alishinda uchaguzi wa rais na mwaka 2017, mwaka wake wa kwanza akiwa madarakani.

Taarifa zikaeleza kwamba katika kupindi cha kati ya miaka 10 iliyotanguli hadi 2016, hakulipa kodi yoyote, kwa kiasi kikubwa kutokana nakuripoti kwamba alipoteza fedha nyingi kuliko alizopata.

Gazeti hilo lilifahamisha kwamba limekusanya rekodi za Trump za kukusanya ushuru kupitia kampuni zake kwa zaidi ya miongo miwili na kubaini kwamba rais huyo amekuwa akikwepa kodi kwa kiasi hicho.

Baada ya Trump kupata taarifa hizo alikimbilia kujibu na kueleza kuwa ni taarifa za uongo zenye lengo la kumchafulia kampeni kuelekea katika mbio za urais.

“Hii ni habari ya uongo, ni uongo mtupu, imetengenezwa. Tutafanya taarifa kama hizo, mngeniuliza maswali kama hayo, miaka minne iliyopita kuhalalisha hili na tukazungumzia hilo. Ni taarifa ya uongo kabisa”, alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa yeye ni mlipa kodi mzuri na kwamba mapato yake yamekuwa yakifanyiwa uhakiki na kukatwa kodi huku akilaumu idara inayohusika na kodi haimtendei vizuri.

Ingawa kwa miaka mingi vyombo vya habari vya Marekani vimekuwa vikihoji kuhusu rais Trump kutolipa kodi, hata hivyo gazeti la New York Times, limeripua bomu jengine.

Kwa mujibu wa taarifa mpya zilizoripotiwa na gazeti hilo gazeti hilo, limebainisha kuwa kati ya mwaka 2013 na mwaka 2015 rais Trump alilipa kiasi cha dola za Marekani 188,561 nchini China.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, malipo hayo yanahusishwa na akaunti ya benki ambayo inamilikiwa na Trump nchini China, ambapo kwa miaka minne angejaribu kutafuta fursa za kibiashara nchini humo.

Akaunti hiyo inasimamiwa na uongozi wa Trump International Hotels na michango yake kwa hazina ya China vina uhusiano na malipo ya kodi nchini humo.

Msemaji wa Trump aliliambia gazeti hilo kuwa akaunti hiyo ilianzishwa kwa ajili ya  fursa muhimu katika sekta ya hoteli barani Asia.’

Tangu kampeni zake za uchaguzi wa mwaka 2016, msimamo wa Trump kwa China kumesababisha hali ya mabishano, ikiwemo kukosolewa kwa makampuni ya Marekani kufanya biashara nchini humo.

Mwezi Agosti mwaka huu, rais huyo alitaka kutoa motisha ya ushuru kwa kampuni za Marekani kuhamisha viwanda vyao kutoka China. Pia alitishia kuondoa mikataba ya serikali kutoka kwa kampuni hizo ambazo zinaendelea kuchukua kazi za China.

Rais alifika ikulu akiituhumu China kuchukua faida ya kibiashara ya Marekani na ameanzisha vita vya biashara, kuwekewa vizuizi kwa kampuni za China kama Huawei kufanya kazi Marekani kama ilivyo tuhuma dhidi ya Beijing kwa kutodhibiti virusi vya corona kwa wakati.

Wakati wa kampeni ya urais ya uchaguzi wa mwezi Novemba, Trump amekuwa akimkosoa sana mgombea wa Chama cha Democrat, Joe Biden, ambaye anasema atakuwa mpole kwa China endapo atachukua madaraka.

Wakati huo huo, ametoa shutuma nzito kuhusu madai ya biashara na Hunter Biden, mtoto wa mgombea wa Joe Biden, huko nchini China.

Si mapato ya ushuru wala katika taarifa za kifedha ambazo Joe Biden ameweka wazi hadharani kuhusu kuwepo kwa dalili za mazungumzo na China.

Alan Garten, wakili wa Shirika la Trump, aliita hadithi ya NYT kuwa “uvumi” na akasema ilizua “mawazo yasiyofaa.”

Garten aliliambia gazeti hilo kuwa uongozi wa Hoteli za Kimataifa za Trump “umefungua akaunti na benki ya China ambayo ilikuwa na ofisi nchini Marekani ili kulipa ushuru wa ndani.”

“Hakuna makubaliano, wala shughuli yoyote au aina nyingine yoyote ya kibiashara iliyotekelezeka na, tangu 2015, ofisi imebaki kimya,” Garten alisema.

“Ingawa akaunti ya benki imebaki wazi, haijawahi kutumiwa kwa madhumuni mengine yoyote,” aliongeza katika mazungumzo yake na NYT.

Trump ana biashara nyingi za nje ya nchi, pamoja na viwanja vya mchezo wa gofu huko Scotland na Ireland na mlolongo wa hoteli za nyota tano.

Kwa mujibu wa The New York Times, Trump ana akaunti za benki nchini China, Uingereza na Ireland.

Gazeti la Marekani lilitoa maelezo ya jinsi Trump alivyotaka kufanya biashara katika nchi hiyo ya Asia, hasa tangu mwaka 2012 alipofungua ofisi huko Shanghai.

Habari ya ushuru kuhusu rais iliyochapishwa na NYT inaonesha kuwa rais aliwekeza kwa miaka kadhaa karibu dola za Kimarekani 192,000 katika kampuni tano ndogo zilizoundwa mahsusi kutafuta biashara nchini China.

Hatahivyo, mipango ya Trump huko China imekuwa chini ya uongozi wa Hoteli za Kimataifa za Trump, kupitia umiliki wa moja kwa moja wa Shirika la Maendeleo ya China ya THC, kwa mujibu wa NYT.