UHASAMA unaoendelea baina ya Ethiopia na Misri, kiasi cha kuwepo mashambulizi ya kijeshi unaelezwa na wachambuzi wengi kwamba unachochewa na rais wa Marekani, Donald Trump.

Misri imeingia kwenye mzozo mkubwa na Ethiopia kufuatia uamuzi wake kujenga bwawa kubwa liitwalo ‘Grand Renaissance’ la kuzalisha umeme katika mto Nile, ikihofia kwamba uzalishaji wa umeme kwneye bwawa hilo utazorotesha utiririshaji wa maji katika mto huo.

Hatua ya rais wa Marekani Donald Trump, kuongeza mvutano kati ya washirika wawili wa Marekani wa muda mrefu, Misri na Ethiopia, kuhusu bwawa kubwa la mto Nile ni ishara ya kufeli kwa diplomasia ya utawala wake barani Afrika.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita, Trump alisema kwamba Misri huenda ikaripua bwawa lililojengwa na Ethiopia, licha ya kujidai mwezi Januari kwamba anastahili kupewa tuzo ya amani ya nobel kwasababu ya machango wake katika utatuzi wa mzozo wa mto Nile.

“Nimezuia kutokea kwa vita. Nimezuia vita mara kadhaa,” alisema, muda mfupi baada ya waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kupewa tuzo hiyo.

Matamshi hayo ya Trump, yalikuwa ya kutatanisha, lakini yalionekana kuashiria jitihada zake za kuingilia kati mzozo huo kupitia ombi la rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi ambaye wakati mmoja aliripotiwa kumuita ‘dikteta wake mpendwa’.

Misri inaona bwawa hilo kama tishio kubwa kwa uhai wake hata kuliko Sudan. Ethiopia, kwa upende mwingine inachukulia bwawa hilo kuwa na umuhimu mkubwa katika mahitaji yake.

Mchambuzi wa masala ya pembe ya Afrika anayeishi nchini Kenya, Rashid Abdi alisema usuluhishi wa Marekani kwa mzozo unaozunguka bwawa hilo umeongeza mvutano zaidi kati ya Misri na Ethiopia.

Kutokana na Trump kutishia Misri huenda ikaliripua bwawa la ‘Grand Renaissance’, taarifa zinaeleza hivi sasa Ethiopia imeanza kuchukua tahdhari kwa kuongeza ulinzi katika eneo hilo.

Grand Renaissance Dam

Kwa sasa Ethiopia imetangaza kwamba eneo la Benishangul-Gumuz, ambapo ndipo panapojengwa bwawa hilo, anga yake imefungwa ambapo ripoti zinabainisha kuwa ulinzi umeongezwa maradufu kwa kufofia shambulizi la ndege za kijeshi kutoka Misri.

Kuongezeka kwa mzozo huo kunaonesha wazi kwamba rais huyo wa Marekani amefeli kwa kiasi kikubwa kung’amua jinsi diplomasia inavyofanya kazi duniani.

“Ana dhana potofu kwamba anaweza kufikia mkataba kama hali inavyofanyika katika ulimwengu wa kibiashara, ndio maana aliachia hazina ya Marekani jukumu la majadiliano, wakati sera ya kigeni inatakiwa kuendeshwa na wizara ya mambo ya nje, matokeo yake yamezidisha hali kuwa mbaya zaidi”, alisema Abdi.

Marekani ililaumu Ethiopia kwa kutokuwa na fikra njema baada ya nchi hiyo kuendelea mbele na mpango wa kujaza maji katika bwawa hilo kabla ya hoja iliyoibuliwa na Misri na Sudan kuhusu mtiririko wa maji katika nchi zao kupata ufumbuzi.

Kutokana na hali hiyo, Marekani iliichukulia hatua Ethiopia kwa kuamua kuipunguzia msaada wa thamani ya dola milioni 100, licha ya kwamba Ethiopia ni mshirika muhimu kwa Marekani katika juhudu za kupambana na wanamgambo wa kiislam katika eneo la pembe wa Afrika.

“Ethiopia inahisi kusalitiwa na Marekani na sasa Trump anaonekana kuwa na kiwango cha chuki na Waethopia wengi”, alisema Abdi alisema na kuongeza kwamba wanatumai Joe Biden atashinda uchaguzi wa urais wa Novemba 3.

Gyude Moore, mtaalamu wa ngazi ya juu wa masuala ya sera katika kituo cha maendeleo ya kimataifa chenye makao yake nchini Marekani, alisema hatua ya utawala wa Trump kupendelea Misri si wa kushangaza kwa sababu lengo lake ni kuiunganisha Israel na mataifa ya kiarabu.

Licha ya kwamba Misri imekuwa na mgogoro wa kidiplomasia kwa muda mrefu na Israel, utawala wa Trump hauna mpango wa kuvuruga mambo zaidi wakati inamhitaji Sisi wakati huu kuisaidia kushawishi nchi nyengine za kiarabu kuitambua Israel.

Lengo lake la Marekani kufanikisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na nchi za Kiarabu pia ilichangia kuamua sera yake kwa Sudan, ambayo imefanyiwa mapinduzi makubwa ya kidiplomasia na Marekani kwa kukubali kurejesha uhusiano wake na Israel.

Endapo Trump, atashinda muhula wa pili, anatarajiwa kuendelea kuishinikiza Ethiopia kutatua suala la Misri na Sudan kuhusu bwawa la Nile na wakati huo huo kuhakikisha Sudan inaondolewa katika orodha ya Marekani nchi zinazofadhili ugaidi.

Moore alisema japo utawala wa Trump utahitaji kupongezwa ikiwa bunge la Marekani litaidhinisha kuondolewa kwa Sudan katika orodha ya ugaidi, uamuzi wake wa kuhusisha hatua hiyo na kutambuliwa kwa Israel itakuwa na athari kwa serikali ya waziri mkuu Abdalla Hamdok, ambayo iliingia madarakani mwaka jana baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashir.

“Suala la kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel limeleta mgawanyiko mkubwa katika jamii ya Wasudan. Huenda ikawa hoja itakayotikisa umoja wa nchi wakati serikali tayari inakabiliwa na changamoto za kiusalama na amani ambayo bado ni dhaifu,” Moore aliongeza.

Hata hivyo, sera mpya ya Trump kwa Afrika inaelezwa kama vita badidi baina ya Marekani na China ambayo kwa sasa ina ushawishi mkubwa barani Afrika.

China imeweka kambi yake ya kwanza ya kijeshi nchini Djibouti, karibu na kambi ya Marekani inayotumiwa kwa mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambowa kislamu nchini Somalia, ngome kuu katika oparesheni yake dhid ya ugaidi Afrika na Yemen.

“Hivi karibuni ndege za kivita za Marekani, zilikuwa zinakuja kutua. Wachina walifanyia majaribio kifaa ambacho kiliwafanya marubani wa Marekani kushindwa kuona pakutua”,alisema Abdi.

“Chini ya utawala wa Trump, Marekani imekuwa mpinzani mkuu wa sera za China lakini China imeendelea kuonesha nguvu zake, hali ambayo ni hatari katika eneo la pembe wa Afrika.

Kama sehemu ya juhudi za kabiliana na ushawishi wa ukuaji wa kiuchumi wa China katika bara hilo, utawala wa Trump ulibuni mpango, wa ustawi wa Afrika mwaka 2018 kama kitovu cha sera zake barani humo.

Aliongeza kuwa uwekezaji wa Marekani barani Afrika awali ilikuwa katika sekta ya mafuta na gesi, lakini uwekezaji huo umeshuka vibaya kutokana na kukua kwa mfumo wa kuzalisha mafuta kutoka kwa miamba nchini Marekani.

Utawala wa Trump ulitenga fedha za kufadhili makampuni yake mwaka 2019 ili zijiimarishe barani Afrika, hata hivyo makampuni hayo yanalalamika kwamba hayawezi kushindana na makampuni ya china yaliyo na fedha.

Utawala wa Trump pia umeamua kuondoa kipengele cha sheria ya nafasi ya ukuaji wa Afrika itakapomalizika mwaka 2025, ilikuwa sera ya Marekani Barani Afrika iliyowekwa utawala wa Rais Bill Clinton, ambayo inazipatia nchi za Afrika nafasi ya kufikia soko la Marekani.

Moore anasema utawala huo umejikita zaidi katika masuala ya kibiashara na tayari imeanza kufanya mazungumzo na Kenya – ambayo ni kitovu cha biashara katika kanda ya Afrika Mashariki ambako China imejenga miundo mbinu ya barabara ambayo Marekani inaamini ina lengo la kuunganisha njia za biashara zitakazoiwezesha nchi hiyo ya mara Asia kujiimarisha barani humo na pia kuwa na ushawishi mkubwa duniani.

“Utawala wa Trump unawaza kufanya kazi na Kenya, ili baadaye itumie vigezo iliyotumia Kenya kufanya kazi na mataifa mengine ya Afrika,” Moore alisema.