WASHINGTON, MAREKANI

 

RAIS wa Marekani, Donald Trump aliupokea mkusanyiko wa mamia ya wafuasi wake katika hafla ya kurejea kwake katika ikulu ya White House na kurejea katika mbio za kampeini ya uchaguzi siku tisa baada ya kusimamishwa kutokana na kuugua ugonjwa wa Covid-19 ambao daktari wake anasema hayuko tena katika hatari ya kueneza. Akisimama katika ukumbi wa ikulu hiyo akiwa amevalia barakoa yake, Trump alihutubia mkusanyiko huo wa wafuasi wake wengi wao pia wakiwa wamevalia barakoa na kusema anajihisi mzima.

Katika hotuba hiyo iliyodumu chini ya dakika ishirini, Trump pia aliwaambia wafuasi wake kujitokeza na kupiga kura na kwamba anawapenda.

Akiwa nyuma ya mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura chini ya wiki nne kabla ya uchaguzi mkuu nchini humo, Trump amekuwa akihesabu siku za kurejea tena katika mbio za kampeini.