WASHINGTON, MAREKANI

RAIS wa Marekani Donald Trump, amerejea tena kwenye kampeni za uchaguzi mkuu kwa kufanya mkutano wa kwanza jimboni Florida siku kadhaa tangu alipogundulika na maambukizi ya virusi vya corona.

Maelfu ya wafuasi wake walisimama bila barakoa, walijikusanyika kwenye mkutano wa nje huko Sanford jijini Florida, ambapo Trump alifanya kampeni ya kwanza kati ya nne zilizopangwa.

Mkutano wa kampeni mjini Florida, jimbo ambalo ni muhimu kwa Trump kushinda, unafungua njia ya mikutano zaidi iliyopangwa kufanyika wiki hii katika majimbo ya Pennsylvania, Iowa na North Carolina.

Aliwaeleza wafuasi wake hao waliohudhuria mkutano huo kwa kusema kuwa afya yake imeimarika na yuko huru kukutana tena na wapiga kura bila ya kuwa na wasiwasi wowote.

Trump anayewania muhula wa pili wa uongozi katika uchaguzi wa Novemba 3 nchini Marekani, alilazimika kukatiza kampeni yake kwa karibu siku 10 kufuatia kuambukizwa virusi vya corona mnamo Oktoba 2.

Rais Tramp pamoja na mpinzani wake Joe Biden, wanapambana ndani ya wiki tatu kufanya kampeni katika kutafuta kura ikifikia uchaguzi mkuu November 3 mwaka huu.

Upigaji kura unaonyesha Biden ana uongozi wa alama 10 juu ya Rais Trump kitaifa, ijapokuwa kuongoza kwake katika majimbo muhimu bado yupo chini, kama inavyoonesha katika jimbo la Florida, ambapo yuko mbele kwa alama 3.7, kulingana na wastani wa kura zilizokusanywa na siasa ya wazi.