KWA muda mrefu sasa Ethiopia na Misri zimekuwa kwenye mzozo mkubwa unaohusu matumizi ya maji katika mto Nile, ambayo umekuwa na umuhimu wa kipekee kwa mamilioni ya wananchi wa nchi hizo.

Mazungumzo baina ya nchi hizo ni kutafuta mustakbali wa kutafuta suluhu ya matumizi ya maji hasa baada ya Ethiopia kuchukua uamuzi wa kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme.

Misri inauchukulia mradi wa uzalishaji umeme katika bwawa hilo la nchini Ethiopia kama tishio kubwa kwa maslahi yake katika matumizi ya maji ya mto kwa wananchi wa nchi hiyo.

Pamoja na kufanya mazungumzo kadhaa ambayo wakati mwengine yalidhaminiwa na Marekani, nchi hizo zimeshindwa kufikia makubaliano hali inayotishia amani baina majirani hao wawili.

Misri, imelichukulia suala la bwawa la Ethiopia kwa umakini mkubwa kiasi kwamba hata imewahi kuziomba nchi za Jumuiya ya nchi za Kiarabu zitajadili suala hilo na ziweze kusaidia kupatikana kwa muafaka.

Misri inailaumu Ethiopia kwa kukosekana mafanikio ya kufikia makubaliano, ikisema kuwa nchi hiyo haina nia thabiti ya kutaka kufikiwa makubaliano ya kisiasa.

Katika moja ya hotuba iliyotolewa na rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi aliwahi kueleza kwamba nchi yake inataka na imeendelea kusimama imara kwa dhati juu ya kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo huo.

Hofu ya Misri ni kwamba bwawa hilo la umeme linaweza kupunguza mtiririko wa maji kutoka kwenye mto wa Nile kuelekea nchini Misri, maji ambayo yanakimu mahitaji ya maji safi ya Misri kwa karibu asilimia 97.

Ethiopia nayo inasema kuwa bwawa hilo linahitajika kwa maendeleo yake na imesisitiza kwamba mtiririko wa maji kuelekea Misri hautaathiriwa katika mto huo unaosambaza maji na umeme kwa nchi 10 ambazo maji hayo yanapitia.

Misiri inautegemea mto Nile kwa shughuli za kilimo, viwanda na matumizi ya maji ya ndani hata, hivyo Ethiopia imesema wasiwasi wa Misri hauna msingi ambapo imetumia dola bilioni 4.8 ya ujenzi wa bwawa hilo ambapo madhumuni yake ni kuzalisha umeme.

Mzozo baina ya Ethiopia na Misri hivi sasa unaonekana kama vile umeshika kasi sana baada ya waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kueleza bayana kwamba rais wa Marekani, Donald Trump kutoa kauli ambayo inachochea vita baina ya nchi hizo majirani.

Ethiopia imemtuhumu rais Trump kwa kuchochea vita kuhusu bwawa la mto Nile baada ya rais huyo kuzungumza dhidi ya mradi huo na kusema Misri inaweza kuuharibu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Gedu Andargachew alimuita balozi wa Marekani Michael Raynor kutoa ufafanuzi juu ya matamshi ya Trump, yanayoashiria hatua ya karibuni ya kujiingiza kwa rais huyo katika mzozo nyeti wa muda mrefu kati ya Ethiopia na mataifa jirani ya Sudan na Misri.

Gedu alimuambia Raynor kwamba uchochezi wa vita kati ya Ethiopia na Misri na rais alieko madarakni nchini Marekani hauakisi ushirikiano wa muda mrefu na ushirika wa kimkakati kati ya Ethiopia na Marekani, na wala haukubaliki katika sheria ya kimataifa inayoongoza uhusiano baina ya mataifa,” ilisema wizara ya mambo ya nje katika taarifa.

Ethiopia ilikuwa inajibu matamshi kuhusu bwawa, maarufu kama Grand Renaissance, yaliotolewa na Trump hivi karibuni wakati wa hafla ya kuadhimisha mafanikio ya kusawazisha uhusiano kati ya Israel na Sudan.

Matamshi hayo yalitolewa saa chache baada ya Trump kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok, na walitoa wito wa suluhu la kirafiki kati ya Ethiopia na Misri.

Katika simu hiyo iliyopigwa mbele ya waandishi habari katika ikulu ya White House, Trump alisema ameipa Misri ushauri huo huo, na kuongeza kuwa hali imekuwa ya hatari.

Aidha Trump ameonya kwamba Misri inaweza kuishia kulilipua bwawa hilo. “Ni hali ya hatari sana kwa sababu Misri haitoweza kuishi namna hiyo,” Trump aliwambia waandishi habari katika ofisi yake ya White House.

“Wataishia kwa kulipua bwawa hilo. Na nilisema na nalisema wazi watalipua bwawa hilo. Na laazima wafanye jambo,” Trump alisema.

Ofisi ya waziri mkuu Abiy ilitoa taarifa ikitetea bwawa hilo na kubainisha kwamba Ethiopia ilikuwa imejifunga kwa mazungumzo yanayoongozwa na Umoja wa Afrika, ambayo ilisema “yamepiga hatua muhimu.”

“Pamoja na hayo, matamshi ya nyakati fulani ya kutoa vitisho ili kuifanya Ethiopia isalimu amri kwa masharti yasiyo ya haki yanaendelea kutolewa. Vitisho hivi dhidi ya mamlaka ya Ethiopia vimeshauriwa vibaya, havina manufaa na ni ukiukaji wa wazi wa sheria ya kimataifa,” ilsiema taarifa hiyo.

Nakala tofuati ya tamko iliyotolewa kwa lugha ya Amharic, ilikuwa na maneno makali zaidi.

“Kuna ukweli wa aina mbili ambao dunia imeuthibitisha. Kwamba hakuja kuwa na mtu alieishi kwa amani baada ya kuichokoza Ethiopia. Wa pili ni kwamba ikiwa Ethiopia inasimama pamoja kwa lengo moja, hakuna shaka kwamba itaibuka mshindi”, lilisema.

Juhudi za Washington kuongoza makubaliano kutatua suala la bwawa ziliishia kwa kushindwa mwaka huu baada ya Ethiopia kuutuhumu utawala wa Trump kwa kuipendelea Misri.

Marekani ilitangaza mwezi uliyopita kwamba inasitisha sehemu ya msaada wake wa kifedha kwa Ethiopia, ikielezea kukosena kwa maendeleo katika mazungumzo na uamuzi wa upande mmoja wa Ethiopia, kuanza kujaza hifadhi ya maji ya bwawa hilo.

Maofisa wengi wa Ethiopia wanamuona Trump kama mtu aliezibwa macho na ushirika wake na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi.

“Samahani kusema haya lakini bwana huyu hajui kabisa anachozungumzia. Ethiopia kamwe haitatishiwa na matamshi ya kizembe kama hayo,” alisema mtangulizi wa Abiy Hailemriam desalegn, katika ujumbe wa Twitter.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, alisema katika taarifa kwamba makubaliano kuhusu bwawa hilo yalikuwa yanakaribiwa kufikiwa.