SIKU ya uchaguzi mkuu iliyosubiriwa kwa muda mrefu hatimaye ndio kesho, ambapo ni muhimu kwa kila mwananchi aliyejiandikisha na kuhakikiwa kwa taarifa zake ajitokeze kwenda kupiga kura.

Hadi kuifikia siku ya kesho ya uchaguzi ya uchaguzi mkuu, mchakato wa zoezi zima ulipitia hatua mbalimbali ikiwemo kampeni, ambazo tunathubutu kusema kuwa ilikuwa fursa muhimu kwa vyama na wagombea kunadi na kuelezea sera zao kwa wananchi.

Tunavyoamini na ndivyo ilivyo, wananchi walizifuatilia kwa makini kampeni hizo kwa kushiriki moja kwa moja kwenye mikutano iliyofanyika katika maeneo mbalimbali na wengine kuzifuatilia kupitia vyombo vya habari.

Tunaamini kesho wananchi watakwenda kwenye zoezi la kupiga kura wakiwa wameshafanya uamuzi sahihi wa kwenda kukichagua chama ama mgombea baada ya kuzielewa na kuzifamu sera.

Kitu kikubwa ambacho tungependa kukusisitiza katika tahariri hii ni kuhakisha wananchi wanajitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na kwenda kukamilisha zoezi zima la haki yao kikatiba.

Kuna faida nyingi za kushiriki kwenye uchaguzi wa hapo kesho, ikiwemo kushirikia kumchagua kiongozi ambaye wewe unaamini kuwa ndiye atakayefaa kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya wananchi wa Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Tunaelewa vipo vitisho na hofu miongoni mwa jamii, lakini tuwaeleze wananchi kwamba suala la ulinzi wako kama mpiga kura na kama mwananchi limedhaminiwa na serikali yako na kwamba huna sababu ya kuwa na hofu.

Unapowaona askari na maofisa usalama wapo kwenye vituo vya kupiga kura wamewekwa kwa ajili ya kukulinda wewe mwananchi na si vyenginevyo, kitu cha muhimu ni kujieleza vizuri.

Chonde chonde katika zoezi hilo la kesho ukisha maliza kupiga kupiga kura huna sababu ya kukaa kituoni kwa ajili ya kulinda kura, hasa ikizingatiwa kuwa jukumu la kulinda kura kwa mujibu wa sheria wanalo watu wengine na wala halikuusu.

Ukweli ni kwamba zoezi zima la uchaguzi litakuwa kwenye amani na hakuna atakayenyukuliwa wala kuguswa, endapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.