NA KHAMISUU ABDALLAH

TUME ya Utangazaji Zanzibar imekifungia kituo cha Maudhui ya Mtandaoni cha RVS Oline TV, kinachomilikiwa na Rashid Almas kwa muda wa miezi miwili mfululizo.

Hatua hiyo, imefatia kituo hicho kukiuka muongozo wa huduma za utangazaji wakati wa uchaguzi mwaka huu kwa kuweka taarifa zinazoashiria uchochezi na chuki za kisiasa miongoni mwa jamii.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Omar Said Ameir, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Kikwajuni.

Aidha alisema kwa mamlaka iliyopewa tume hiyo na sheria ya tume namba 7 ya mwaka 1997 chini ya kifungu cha 16 (e) imesitisha leseni ya utangazaji ya kituo hicho kwa muda huo kuanzia jana hadi 21 Disemba 2020.

Alisema tume ilitoa muongozo wa huduma za utangazaji wakati wa uchaguzi 2020 unaovitaka vyombo vya utangazaji vikiwemo redio, television na maudhui ya mtandaoni kufuata kikamilifu maadili hayo katika kutangaza matangazo ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuweka usawa katika kufanya vipindi na matangazo ya kampeni za uchaguzi.

Katibu huyo alisema tume baada ya kufanya ufatiliji wa vituo vyote vya utangazaji vilivyosajiliwa imegundua kituo hicho hakitoi uwiano ulio sawa kwa vyama vyote vya siasa, na baadhi ya maudhui yanayorushwa yanaashiria uvunjifu wa amani na uvunjifu wa sheria za nchi.

Alisema kufanya hivyo ni kinyume na kifungu namba 5(i) cha muongozo wa huduma za utangazaji wakati wa uchaguzi Zan zibar 2020 na kifungu 14 (i) cha kanuni ya maudhui ya mtandaoni ya mwaka 2019.

Alibainisha kwamba Disemba 21, mwaka huu mmiliki wa kituo hicho aliitwa na tume kwa ajili ya kujibu hoja za kukiuka mwongozo wa huduma za utangazaji wakati wa uchaguzi 2020 kwa kuweka video ya maudhui ya siasa ambayo chama kimoja haikuwa na ubora.