NA ABOUD MAHMOUD

MICHEZO ni moja ya sekta muhimu sana katika nchi ambayo inasaidia kujitangaza kitaifa na kimataifa, wakati wananchi wanapoziwakilisha nchi zao.

Lakini pia michezo husaidia katika kujenga afya ya mwanadamu na kumuepusha na maradhi mbali mbali, ambayo hutokana na kukaa bila kufanya mazozei ya aina yoyote.

Lakini katika ulimwengu wa leo michezo imefika mbali mbali kwa vile hivi sasa michezo imekuwa sehemu ya ajira kwa watu werngi sana duniani, kwani imeweza  kuwasaidia wananchi wa dunia nzima kufaidika kwa kupata mafanikio ya maisha  kwa kpa mishahara mikubwa tofauti na miaka ya nyuma.

Zanzibar ni miongoni mwa nchi ambazo michezo imesaidia kujitangaza kitaifa na kimataifa, lakini pia katika maswala ya ajira vijana wengi wamepata ajira katika idara mbali mbali zikiwemo za serikali na binafsi .

Hili ni jambo jema kwani vijana wengi ambao wamekuwa na kilio cha siku nyingi cha ajira, wamefanikiwa kufikia ndoto zao walizokua nazo katika kujipatia maendeleo kupitia fani hiyo.

Hivi karibuni Balozi wa Heshima wa  Jamhuri ya Brazil Zanzibar, Abdulsamad Abdulrahim alionesha nia ya kusaidia michezo mbali mbali, ikiwemo mpira wa kikapu, soka la ufukweni na kapoeira wenye asili kutoka nchi hiyo.

Msaada wake katika michezo hiyo ni pamoja na kuwasaidia wachezaji kupata vifaa, kushiriki katika mashindano ya kimataifa, kufanyika kwa mashindano ya mara kwa mara, kuwajengea uzoefu makocha na wachezaji pamoja na kuvifanyia ukarabati viwanja vya michezo.

Kufanya hivyo ni dalili nzuri ambazo zinaonesha kuwajengea uwezo na ufanisi wanamichezo wa Zanzibar ambao wamekua na kilio cha muda mrefu kutaka kufika mbali.

Lakini mbali na kuwajengea uwezo wanamichezo nchini pia ni dalili tosha ya kiongozi ambae anaonesha nia thabiti ya kuwajali Wazanzibari, kushiriki katika mashindano ya kimataifa ambayo yataweza kuiweka nchi katika ramani ya dunia.

Ni faraja kubwa kwa wanamichezo wa Zanzibar hususan nilioitaja hapo awali kwani ni muda mchache wataanza kuona matunda ya ushiriki wao wa michezo kutoka kwa Balozi huyo.

Vyema tufahamu kwamba kiongozi huyo ambae ni mzalendo na amekuwa na hamu ya kutaka kuona Zanzibar, inafikia malengo yaliokusudiwa katika kukuza michezo ni vyema juhudi zake zisibezwe.