NA KHAMISUU ABDALLAH
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema CCM inafanya kampeni kwa kujitegemea wenyewe, nidhamu, ilani ya chama ya 2020/2025 na kuwa na wagombea wanaofika muda wa mwisho wa uchaguzi.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na wazee wa Chama cha Mapinduzi katika Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui ikiwa ni agizo la kamati ndogo ya Halmashauri Kuu kilichofanyika Oktoba 4 chini ya Makamo Mwenyekiti wa CCM Dk. Ali Mohammed Shein.
Alisema, dhana hizo zinatokana na waasisi wa Tanzania akiwemo marehemu mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Nyerere kuwa na maono ya nchi ijitegemee wenyewe.
Aidha alisema CCM inafata maelekezo ya kutii sheria za nchi maadili ya uchaguzi na nidhamu katika kuendesha uchaguzi na kampeni za kistaarabu.
“Tumetukanwa sana kwa kuitwa vinyago, wajinga na majina mengine na kuchonganishwa na watu lakini hatukujibu. Dhambi yetu ni kuona tunawaunganisha watanzania, kuulinda muungano na mapinduzi, kupambana na ubaguzi na kuhakikisha tunashinda ndio dhambi yetu kubwa,” alisema.
Alisema ikiwa CCM itafanya mambo yanayofanywa na wapinzani basi itapoteza nidhamu na kusaliti urithi wa wazee na waasisi wa taifa Mwalimu Nyerere na mzee Abeid Amani Karume.
Dk. Bashiru alisema, yapo matukio ya kuuawa kwa watu na wengine kujeruhiwa kwa kisingizio cha siasa mambo ambayo hayakubaliki kisheria.
Hivyo, aliwaomba viongozi wa dini kulinda nyumba za ibada dhidi ya chuki na fitna zinazotokana na watu kwa kisingizio cha siasa.
“Tuna mungu mmoja hatuna mungu mwengine wa siasa na chuki kwani jambo hili ni ishara mbaya na sio utanzania kwani tunahitaji kujifunza,” alisema.
Aliwataka vijana kujifunza kutoka kwa wazee waliojitokeza kumwaga jasho lao kwa ajili ya Taifa la Tanzania kwa kuendeleza amani ya nchi yao katika kipindi chote cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Mbali na hayo Dk. Bashiru, alisema CCM inatambua mchango wa Baraza la Wazee Afisi kuu kwani ndio baraza pekee la kitaifa linalotoa mchango mkubwa kwa chama chao.