HALI halisi ya ugumu wa ajira inazikabili nchi mbali mbali, zaidi ikiwakumba vijana hali ambayo inatulazimisha tuzidi kuumiza vichwa ili tuweze kupata mikakati mizuri na endelevu ya kuunda fursa za ajira.

Uhaba wa ajira umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka wimbi la wakimbizi kutoka nchi moja hadi nyengine, lakini pia kusababisha matatizo makubwa ya ndabni ya nchi, ikiwemo vijana kuhamia mijini kwa wingi.

Katika siku za hivi karibuni tumekuwa tukiona picha za vijana wa kiume, wanawake na watoto wakikumbwa na matatizo makubwa, ikiwemo kuzama baharini na kupoteza maisha wakati wakivuka bahari kwenda kutafuta maisha bora Ulaya. 

Katika mazingara ya nchi zetu zinazoendelea ikiwemo Zanzibar, nasi hatuna budi kujiandaa zaidi katika kuepuka majanga kama hayo yasijewafika vijana wetu.

Ni dhahiri viwanda iwe vikubwa au vidogo ndio sekta yenye umuhimu na fursa za kipekee katika kuunda ajira nyingi zaidi katika nchi yoyote ile, ikiwa ni pamoja na Zanzibar.

Kuna wakati Zanzibar tulikuwa na viwanda kadhaa vilivyo kuwa vikimilikiwa na serikali, ambavyo licha ya kuzalisha bidhaa muhimu zilizohitajika sana, pia viwanda hivyo ambavyo vingi sasa havifanyi kazi viliajiri wananchi wengi.

Serikali inafahamu mchango wa viwanda ndio maana imekuwa ikitoa kipaumbele katika sekta za biashara, kilimo na viwanda ambazo zinategemeana sana. Ingawa ni ukweli kwamba kwa upande wa viwanda hadi sasa Zanzibar haijafikia hatua ya kutegemea sekta hiyo.

Baadhi ya wawekezaji wameweza kujitutumua kwa kuanzisha viwanda vidogo na kuwapatia vijana na wananchi mbali mbali ajira, lakini licha ya uhaba wa wananchi Unguja na Pemba, ambao hawazidi milioni moja na nusu, bado juhudi zinahitajika zaidi kuinua sekta ya viwanda.

Lakini kwa kuwa ujenzi na uanzishwaji wa viwanda huhitaji rasilimali na uwezkezaji mkubwa, wakati huu juhudi za kukuza sekta hiyo zikiwa zinaendelea, sekta nyengine nazo zipewe umuhimu wa kipekee kuunda ajira za kutosha.

Tafiti mbali mbali zilizofanywa bado zinaonesha uhaba wa ajira ni tatizo kubwa Zanzibar, kama ilivyo kwa Tanzania kwa jumla pamoja na nchi nyengine nyingi Barani Afrika.     

Kwa sasa lazima tuwe wabunifu katika miradi kama kuendeleza kilimo cha kisasa na ujasiriamali wa aina mbali mbali, maeneo ambayo yamethibitika kutoa fursa nyingi kwa vijana na kina mama kujipatia fursa za kukuza uchumi.

Bila shaka yoyote ile vijana wataweza kushajiika sana na ajira za aina hii, badala ya kusubiri kuajiriwa na Serikali. Vijana ninao wazungumzia ni waliomaliza masomo vyuoni na hata wale ambao hawakusoma, ambao bado wako mitaani bila ya kazi.