UCHAFUZI wa hali ya hewa ni kuchanganyika kwa hewa asili katika anga na vitu kama vile moshi, jivu, gesi za kemikali na kadhalika hali ambayo huathiri sifa ya hewa na kusababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine.

Katika daraja lililokaribu zaidi na ardhi, anga huwa mkusanyiko wa gesi za nitrojeni, oksijeni, kabon dioksidi na gesi nyingine katika viwango vidogo.

Lakini katika anga za juu zaidi kuna tabaka ya ozon ambali hukinga miale ya jua inayoweza kusababisha madhara kutoingia katika sayari ya dunia.

Vipo baadhi ya vitu vinavyofanywa na wanaadamu husababisha kuathirika hali hewa ikiwemo moshi unatoka kwenye viwanda, moshi kutoka kwenye gari, dawa za kuuwa wadudu na kadhalika.

Suala la uchafuzi wa hali ya hewa limekuwa kwenye ajenda ya dunia, huk nchi zinazoongoza uchafuzi zikishindikizwa kuhakikisha zinapunguza shughuli zinazochafua hali ya hewa.

Nchi zinazozalisha hewa chafu zinahofia endapo zitadhibiti uzalishaji wa hewa hizo kuna uwezekano wa kuyumba kiuchumi, hata hivyo athari za machafuko ya hali ya hewa zinasababisha athari kubwa kwa nchi ambazo hazizalishi hewa chafu.

Uchafuzi wa hewa unaelezwa kuwa ni uuaji wa taratibu, ambapo ni vigumu sana kubaini kwamba tatizo hilo linasababisha vifo vya mamilioni ya watu ulimwenguni.

Kwa mujibu wa mmoja wa wataalamu wa uchafuzi wa hali ya hewa David Boyd, amebainisha kuwa tatizo hilo linaharakisha vifo vya mapema vya watu milioni saba kila mwaka.

Alibainisha kuwa wengi wanaofariki kutoka na mchango wa uchafuzi wa hali ya hewa ni wanawake na watoto kutoka katika jamii maskini masikini ulimwneguni, ambapo kwa takwimu hizo maana yake ni kwamba kila kila sekunde tano mtu mmoja kufariki kutoka na changamoto hiyo.

Boyd alisema kwamba kushindwa kuhakikisha uwepo wa hewa safi ni kinyume na haki ya binadamu ya uhai, afya na ustawi pamoja na haki ya kuishi katika mazingira yenye afya.

Alisisitiza kuwa haki ya mazingira yenye afya ni msingi wa ustawi wa binadamu na inatambuliwa na zaidi ya mataifa 150 katika ngazi ya taifa na kikanda hivyo haki hiyo inapaswa kupatiwa msisitizo kimataifa ili kuhakikisha haki hii inafurahiwa na kila mtu, popote alipo.

Utafiti uliofanywa unaonesha kuwa maelfu ya watoto wachanga, na hasa India na mataifa ya Afrika katika eneo la Kusini mwa Sahara kwa mwaka 2019 wamekufa kutokana na uchafuzi wa hewa.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kiini cha vifo hivyo vinavyotokana na uchafuzi wa hali ya hewa ni moshi wenye sumu.

Idadi watoto wachanga wanaokadiriwa kufikia 476,000 kote ulimwenguni walifariki kutokana na athari mbaya za zinazotajwa kutokana na uchafuzi wa hewa katika kipindi cha 2019.

Utafiti huo ambao unajikita katika utambuzi wa mazingira ya dunia, ambao umetolewa hivi karibuni, unasema theluthi mbili ya vifo hivyo vilivyotajwa, vinahusiana na kwa mafuta yenye kiwango duni yanayotumika kama nishati ya upishi wa majumbani.

Rekodi za utafiti huo mpya zinaonesha watoto wachanga wapatao 236,000 wanakadriwa kufa kwa sababu zinazohusiana na uchafuzi wa hewa barani Afrika katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara na zaidi ya wengine 116,000 nchini India.

Nchi ya Pakistan pia inatajwa kuwa na zaidi ya vifo vya watoto wachanga 50,000 kutokana na kadhia hiyo ya uchafuzi wa hewa.

Kulingana na utafiti huo, kina mama wanapokumbwa na uchafuzi mkubwa wa hewa, inaweza kuleta hatari kubwa ya watoto wao, ambapo wanaweza kuzaliwa wakiwa na uzito mdogo au kuzaliwa kabla ya wakati kwa maana ya watoto njiti.

Hali hiyo kimsingi inaweza kusababisha au kuongeza hatari ya watoto kufa katika mwezi wa mwanzo wa maisha yao, lakini pia kuwa na athari mbaya kwa afya yao kwa maisha yote endapo walinusurika utotoni.

Ingawa utafiti huo ulibaini kwamba asilimia 64 ya vifo vilitokana na uchafuzi wa hewa majumbani, lakini uchafuzi wa mazingira kwa ujumla wake pia ulichukua nafasi kubwa, haswa Kusini mwa Asia.

Katika maeneo hayo asilimia 50 ya vifo vya watoto wachanga vilihusishwa na athari ya uchafuzi wa hewa kutoka nje ya nyumba zao yaani ikujumisha mazingira yanayowazunguka.

Kwa mujibu wa utafiti huo, uchafuzi wa hali ya hewa kwa ujumla ulisababisha vifo milioni 6.7 ulimwenguni kote katika kipindi hicho cha mwaka 2019, ambapo kiwango hicho kinaufanya uchafuzi wa hewa kuwa sababu ya nne inayoongoza kwa vifo vya mapema kabla nyingine ambazo ni shinikizo la damu, matumizi ya tumbaku na lishe duni.

Waandishi wa utafiti huo mpya kuhusu hali ya hewa duniani wamegundua kwamba kumekua na hatua kidogo zilizopigwa katika kukabilana na tatizo hilo katika baadhi ya maeneo hapa ulimwenguni.

Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa yapo maneno mengine hakuna kabisa kilichofanyika katika jitihada za kupunguza uchafuzi wa hewa katika maeneo mengi ya ulimwengu, licha ya kuwepo ushahidi unaoongezeka katika kuonyesha athari zake kwa afya ya binadamu.

Miongoni mwa mambo mengine, wamesema kwamba kutokea kwa athari zitokanazo na uchafuzi wa hewa kwa kipindi fulani kunaweza kusababisha sio tu hali mbaya ya kiafya, bali pia kuwafanya watu wawe katika hatari zaidi ya kupatwa na uogonjwa wa COVID-19 katikati ya janga la sasa linaloendelea kuisumbua dunia.