NA MWANDISHI WETU
UCHAFUZI wa fukwe katika ukanda wa pwani unaweza kupoteza hadhi ya biashara ya utalii kutokana na umuhimu wake kama miongoni mwa vivutio vikubwa vinavyowavutia watalii wengi zaidi kutembelea visiwa vyetu vya Unguja na Pemba.
Yako wapi yale makundi ya ndege weupe maarufu kama ndege wa pwani ama yange yange sauti zao zikihamaniza mawimbi ya bahari hadi ufukweni kwa madaha na faraja unapokuwa na msongo wa mawazo.
Inanikumbusha utotoni hasa nyakati za jioni ninapoelekeza macho yangu kwenye usawa wa bahari huku nikiakisi na kutafakari ugumu wa maisha najikuta roho burudani.
Upepo mwanana wa miti ya pwani ikiwemo mikoko, mikadi, milakasa, vitunguu vya pwani, hauvumi kama uvumavyo zama zile ukapata misitu ya asili inayokupa furaha wakati wa majonzi.

Kwa kweli inasikitisha kama si kuhudhunisha fukwe zetu zimekuwa zikiharibiwa kila uchao na hata kugeuzwa kuwa jaa la taka.
Kwa nchi kama Zanzibar ambayo inazidi kupanda chati kwenye sura ya dunia kwa ubora wa viwango vya uendeshaji wa biashara ya utalii hadi kufikia kujulikana kama “Kisiwa cha fukwe nyeupe, yaani “white sand or soft beach island”.
Mjadala huu ni vyema kujadiliwa kwa kina na kuundiwa mikakati imara ili kunusuru fukwe zetu ambazo kwa wakati huu zina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi yetu.
Mwekezaji mzalendo wa mahoteli ya kitalii Abdulsamad Said Ahmed ambaye anasema tatizo la utupaji wa taka ovyo kwenye bahari na fukwe zake linaweza kuleta athari kwenye sekta ya utalii.
Aidha amezitaka mamlaka husika kulipatia ufumbuzi jambo hilo ikiwemo kutoa elimu kwa jamii hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa chupa za plastiki zimezagaa ovyo baharini na kusabisha uchafuzi wa mazingira.
Wananchi kwa upande mwengine nao kwa kutotilia maanani umuhimu wa fukwe zetu wamegeuza kuwa jaa la kutupia taka ngumu na wakati mwengine hata vinyesi jambo ambalo kimtazamo athari zake ni kubwa kama si leo ni kesho, ni dhahiri kuwa fukwe safi zenye kuvutia zinapendezesha si kwa mtalii tu bali hata mzawa kama nilivyozungumza hapo mwanzoani mwa makala haya.
Hii pia inanikumbusha mwaka 2004 ambapo mzungu mmoja alifika kijiji cha Jambiani wilaya ya Kusini Unguja watu walimshangaa wakati akiokota taka huku akizitia kwenye mapolo.
Wapo baadhi ya wakaazi wa Jambiani walimdhihaki na kumcheka kumbe walikuwa wakijicheka wenyewe kwa sababu hawakuwa na uwelewa wa athari za mazingira. Ama kweli jambo usilolijua sawa na usiku wa giza.
Baada ya mzungu yule kuhojiwa kwanini alikuwa anafanya kile kilichoonekana kama kioja, alijibu kwa wepesi tu kwamba itatuchukua miaka mingi kujua umuhimu wa hilo jambo.
Hii ilinipa mawazo kwamba kumbe tumejaaliwa rasilimali ya bahari na fukwe nzuri za kuvutia, lakini hatuoni thamani yake ndio maana tunazichafua kwa kutupa taka.
Aliwaambia waendelee kumcheka iko siku watamkumbuka, kubwa zaidi aliwataka vijana waanzishe Jumuiya za kuhifadhi mazingira kwa faida yao na vijazi vijazo.
Hilo likawa somo tosha kwetu, tulilala usingizi wa pono mpaka mzungu alipotuamsha ndipo wazo la kuanzisha Jumuiya ya Uhifadhi wa Mazingira ya Fukwe na Bahari Jambiani (JAMABECO) lilipozaliwa.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mohamed Okola anasema uchafuzi wa bahari na fukwe zake ni jambo ambalo halijapewa kipaumbele kwa jamii za ukanda wa pwani ambapo elimu endelevu inahitajika kutolewa kwa kuwa fukwe ni vivutio vyetu vya utalii.
Biashara ya utalii haiwezi kukua bila ya kuwepo mandhari nzuri ya kuvutia, kwani wageni au watalii wengi, wanaotembelea katika Visiwa vya Zanzibar wanataraji kujionea mazingira halisi ili iwe kama zawadi ya kusimulia wafikapo makwao.
Hebu na tujiulize hatuoni faida ya utalii? Faida ipo kubwa ikiwemo kutoa ajira kwa watu wa ukanda wa pwani ambapo takribani asilimia 70 ya wanaofanya kazi za hoteli wana makaazi mazuri na hata usafiri mzuri tofauti na miaka ya 1980 ambapo biashara ya utalii ilikuwa haijashika kasi kama sasa.
Utalii una mchango mkubwa kwa uchumi wetu unashika nafasi ya juu kwa asilimia 27 pato la taifa, asilimia 80 fedha za kigeni zinatokana na biashara ya utalii. Utalii ni nguzo kuu kwa uchumi wa Zanzibar na umepelekea ajira 22,000 ajira za moja kwa moja na ajira 48,000 ambazo si za moja kwa moja.
Tuseme tu mara nyingi viongozi wetu wa serikali hutembelea maeneo ya fukwe na kujionea hali ya uharibifu ulivyo, bado hatua stahiki za kuwabana waharibifu hao hazijachukuliwa kikamilifu.
Kwani licha ya utupaji wa taka tatizo la uchimbaji mchanga kwenye fukwe tatizo linazidi kukua siku hadi siku na sidhani kwa uoni wangu mfupi kama watalii watapendezeshwa kuja kuangalia mashimo ya fukwe zetu.
Kamisheni ya Utalii Zanzibar, iliwahi kusema kuwa itawachukulia hatua za kisheria wananchi wanaofanya hujuma katika fukwe za bahari kwa uchimbaji wa mchanga kwani kufanya hivyo ni kuondoa haiba na kutapelekea kushusha kipato katika sekta ya utalii.
Lakini cha kusikitisha baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na bahari huzitumia vibaya fukwe kwa kuzifanyia uharibifu na kusababisha fukwe zile kuharibika na kupoteza ubora wake.
Hata hivyo, serikali za wilaya na Mikoa kwa kushirikiana na Vikosi vya SMZ bado wana nafasi kubwa ya kuzisimamia na kuzifanyia ulinzi kwa umakini mkubwa fukwe ili kuzinusuru na uharibifu huo kwani utalii wa Zanzibar unategemea fukwe katika mapato yake.
Inasemekana kwamba uharibifu huo umekuja mara baada ya serikali kuzuia uchimbaji wa mchanga na wananchi kuhamia katika fukwe za bahari hivyo ametoa wito kwa wananchi kuwacha tabia ya uharibifu na badala yake kuzilinda kwani faida yake ni kubwa katika taifa na hata wao wenyewe.
Kwa upande wake Juma Mahamoud Jaribu (Mabodi) mkaazi wa Jambiani anasema hali imekuwa mbaya kwani mchanga wa pwani unaonekana ni bidhaa muhimu tokea pale serikali ilipozidisha bei ya mchanga kiasi kwamba watu wengi wa sehemu za ukanda wa pwani huchimba mchanga kwa ajili ya kujengea.
“Kasi ya uchimbaji wa mchanga kwenye fukwe inachangiwa na kupandishwa kwa bei ya mchanga wa kujengea huko Mjini, hivyo kwa huku kwetu mchanga wa pwani huuzwa kwa bei nafuu kwani madereva wa gari hujichotea tu bila kulipa kodi kama ilivyo kwa wachukuaji wa mchanga kwenye mashimo yaliyotengwa na serikali, pia wapo mtu mmoja mmoja ambao huchota kwa vipolo mchana kweupe kwa ajili ya kujengea”, alipaza sauti Mabodi.
Tafiti mbali mbali zilizowahi kufanywa na wataalamu na hata ushahidi wa macho upitapo sehemu za ukanda wa pwani kama Jambiani, Paje, Bwejuu, Michamvi, Uroa, Nungwi na kwengineko hali ya fukwe zetu zinakabiliwa na mmong’onyoko mkubwa wa ardhi kunakosababishwa na mlolongo wa mambo ikiwemo ujengaji wa hoteli za kitalii karibu na bahari na uchimbaji mchanga.
Mabadiliko ya tabia nchi nayo yamekuwa yakiruhusu mawimbi makubwa ya maji kupiga hadi kwenye hoteli kiasi kwamba kila muwekezaji anajaribu kujihami kujenga ukuta mkubwa kuzuia hali hiyo. Jambo hili linahitaji utaalamu wa hali ya juu kuliko kila mmoja kufanya atakavyo.
Nchi yetu inategemea zao la karafuu ambalo ni la msimu itategemea pia kiwango cha uzalishaji na soko la dunia lilivyo, sekta inayoweza kutunusuru ni ya utalii pekee ikiwemo vivutio vyake moja wapo ni fukwe, tunapoziharibu ni kwa faida ya nani?
Iwapo kila siku tunaendelea kuchafua mazingira ya fukwe na bahari pamoja na kuchimba mchanga athari yake, ni mmong’onyoko wa fukwe na hatimae hata hayo majengo ya makumbusho yanayowavutia watalii, yanaweza kuathiriwa na majanga yatokanayo na bahari tusipokuwa makini katika kuyaenzi mazingira yetu.
Ni jukumu letu sote kuvilinda vivutio vya utalii ili kuitangaza Zanzibar kuwa kimbilio na sehemu sahihi ya watalii kutembelea na kuongeza pato la taifa letu.