NEW DELHI,INDIA

UCHAFUZI wa hali ya hewa mwaka 2019 uliua watu milioni sita na laki saba kote duniani, wakiwemo watoto wadogo wa kuzaliwa zaidi ya 476,000.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya utafiti uliofanywa wa hali ya hewa duniani State of Global Air 2020 ambapo India na nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika zinaongoza.

Kwa mujibu wa utafiti huo, miongoni mwa watoto wadogo karibu laki tano waliopoteza maisha chini ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa mwaka jana, 116,000 miongoni mwao ni wa India, huku zaidi ya vifo 236,000 vikiripotiwa katika nchi za chini ya jangwa la Sahara.

Kwa ujumla, waliofariki dunia kote duniani mwaka jana kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na taasisi za  athari za Afya (HEI) na  tathmini ya magonjwa za Marekani, ni watu milioni sita na laki saba.

Utafiti mwengine uliofanywa mwaka jana na Chuo Kikuu cha Utah mjini Salt Lake nchini Marekani ulibainisha kuwa, uchafuzi wa hali ya hewa duniani ulipelekea kuongezeka idadi ya mimba kuharibika au wanawake kujifungua kabla ya wakati.

Umoja wa Mataifa umewahi kutahadharisha kuhusu ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa na athari zake kwa viumbe kote duniani, ambapo Marekani ilitajwa kuwa ya kwanza kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda kwa kuchafua mazingira na hali ya hewa.

Pamoja na hayo Rais Donald Trump wa Marekani aliiondoa nchi hiyo katika Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris licha ya malalamiko makubwa ya jamii ya kimataifa.