NA TATU MAKAME

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe ya maulid ya kuzaliwa kwa Mtume (S.A.W), Oktoba 18 mwaka huu.

Maulid hayo yatafanyika katika viwanja vya Maisara mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo viongozi mbali mbali wa vyama na serikali watahudhuria.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa na mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, mke wa Rais wa Zanzibar mama Mwanamwema Shein, mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mama Asha Suleiman Iddi, mke wa mgombea wa urais wa Zanzibar mama Maryam Mwinyi.

Viongozi wengine ni Mawaziri na Manaibu waziri wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Masheikh, maimamu, walimu wa madrasa na wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya kur-an kutoka Zanzibar na Tanzania bara.

Akizungumza na mwandishi wa habari, Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema sherehe hizo zimerejeshwa nyuma kutokana na kuingiliana na harakati za uchaguzi ambao utafanyika Oktoba 28 mwaka huu.

“Mwaka huu tutasherehekea siku ya uzawa wa mtume mwezi Mosi mfunguo sita maana mwezi 11 itakuwa mkesha wa siku ya uchaguzi,” alisema.

Alisema kamati inayohusika na sherehe hizo imeamua kuweka siku hiyo ili kutimiza sherehe hizo kabla ya siku ya uchaguzi.

“Kwa vile mfunguo sita utakuwa umeingia tumeona tusherehekee siku hiyo kwani siku iliyozoeleka ni siku ya kuamkia mkesha wa siku ya uchaguzi,” alisema.

Aliwataka wananchi kufika kwa wingi kuungana na wenzao kusherehekea siku hiyo katika maadhimisho hayo.

Aidha aliwataka wananchi ambao watasherehekea uzawa wa kuzaliwa kwa mtume katika mitaa mbalimbali kuangalia mipaka na kuacha kutumia muda huo kwa mambo mengine mengine kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

“Wale wanaoendeleza sherehe za maulid katika mitaa mbalimbali tunawaomba wamalize shughuli zao mapema ili warudi katika majumba yao wakapumzike, tusitumie wakati huo kufanya mambo ambayo yanakwenda kinyume na maamrisho ya Mtume,” alisema.