Thomas Partey
ARSENAL imekamilisha usajili wa Thomas Partey kutoka Atletico Madrid kwa mkataba wa muda mrefu baada ya kulipa pauni milioni 45.3 za kifungu cha ununuzi wake.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 raia wa Ghana aliichezea Atletico Madrid mara 35 na kufunga magoli matatu na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya tatu katika ‘La Liga’.

Lucas Torreira
KIUNGO wa kati wa Arsenal, Lucas Torreira amebadilishana na Partey na kujiunga na Atletico Madrid kwa mkopo.

Edinson Cavani
MANCHESTER United imemsaini aliyekuwa mshambuliaji wa Paris St Germain, Edinson Cavani kwa uhamisho wa bila ya malipo.
Cavani (33), alifunga magoli 341 katika mechi 556, ikiwemo rekodi ya magoli 200 katika mechi 301 akiichezea miamba hiyo ya Ufaransa.
Pia ana magoli 50 akiichezea timu ya taifa ya Uruguay katika mechi 116.
Mechi yake ya kwanza akiichezea United inaweza ikawa dhidi ya klabu yake ya zamani PSG katika Ligi ya Mabingwa Ulaya mnamo Oktoba 20.

Federico Chiesa
JUVENTUS imemsaini winga wa Italia, Federico Chiesa kutoka Fiorentina katika makubaliano ambayo huenda yakawa na thamani ya pauni milioni 54.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 anajiunga na mabingwa hao wa Italia kwa mkopo wa miaka miwili kabla ya uhamisho wa kudumu.
Chiesa alipitia klabu ya vijana ya Viola kabla ya kuandikisha kandarasi ya kudumu.

Chris Smalling
AS Roma imemsajili beki wa Manchester United, Chris Smalling kwa mktaba wa miaka miwili ulio na thamani ya pauni milioni 13.6 ikipanda hadi euro milioni 20 pamoja na marupuru.
Shirikisho la soka nchini Itali liliandaa stakhabadhi ya uhamisho huo dakika moja kabla ya kukamilika kwa dirisha la uhamisho.

Matteo Guendouzi
KIUNGO wa Arsenal, Matteo Guendouzi amejiunga na klabu ya Bundesliga ya Hertha Berlin kwa mkopo wa kipindi chote cha msimu uliosalia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 hajaichezea Arsenal tangu waliposhindwa 2-1 na Brighton mnamo mwezi Juni ambapo alihusika katika mgogoro na Neal Maupay.
Mchezaji huyo wa Ufaransa alijiunga na Arsenal kutoka Lorient mwaka 2018, baada ya kuanza soka yake katika chuo cha mafunzo ya soka cha PSG.

Rayan Ait-Nouri
KLABU ya Wolverhampton Wanderers wamemsajili mchezaji wa timu ya Ufaransa isiozidi umri wa miaka 21, Rayan Ait-Nouri, huku beki wa timu hiyo, Ruben Vinagre akijiunga na Olympiakos.
Ait – Nouri mwenye umri wa miaka 19 anajiunga katika uhamisho wa muda mrefu kutoka klabu ya Ligue 1 ya Angers.

Raphinha
LEEDS United imekamilisha uhamisho wa winga Raphina kutolka klabu ya Rennes kwa dau linaloaminika kuwa pauni milioni 17 pamoja na marupurupu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 raia wa Brazil ametia saini kandarasi ya miaka.

Ben Godfrey
EVERTON imemsajili beki, Ben Godfrey kutoka Norwich City katika makubaliano yalio na thamani ya pauni milioni 25, ambayo huenda yakaongezeka hadi pauni milioni 30.
Godfrey (22) anajiunga na Toffees katika kandarasi ya miaka mitano. Ni mchezaji wa tano wa Everton kusajiliwa baada ya viungo wa kati Allan na Abdoulaye Doucoure, kiungo mchezeshaji James Rodriguez na beki wa kushoto Niels Nkounkou.