PARIS, UFARANSA

RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron, ametangaza amri ya kutotoka nje wakati wa usiku huko Paris na miji mingine nane, katika juhudi zake za kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Rais Emannuel Macron wa Ufaransa alisema, marufuku hiyo itakuwa kati ya saa tatu usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi na itudumu kwa hadi muda wa wiki sita.

Macron alisema lengo la hatua hiyo ni kupunguza maambukizi ya ‘COVID-19’, kutoka wastani wa visa vya sasa ambavyo ni 20,000 kwa siku hadi angalau kufikia visa 3,000 au 4,000 idadi ambayo inaweza kudhibitiwa.

Kiongozi huyo amesema ingawa Ufaransa haijashindwa kudhibiti janga la corona, ambalo tayari limewauwa watu 29,000 nchini humo, lakini anatiwa wasiwasi na wimbi la maambukizi linaloendelea kuitikisa nchi hiyo.

Wakati huo huo Ujerumani ilitangaza kuwa baa na mikahawa katika maeneo yenye hatari zaidi lazima ifungwe mapema, hii ni kutokana na nchi hiyo kurikodi zaidi ya maambukizo mapya 5,000 kwa mara ya kwanza tangu Aprili.

Hivyo Kansela Angela Merkel alitangaza vizuizi vikali, katika maeneo ambayo huzidi maambukizo 50 kwa wakaazi 100,000, baa na mikahawa lazima ziifungwe 5:00 usiku, na mikusanyiko ya kibinafsi itazuiliwa kwa watu 10 kutoka pande mbili.

Nchi nyingi za Ulaya zinaanzisha vizuizi vipya ili kupambana na wimbi la pili la maambukizo ya corona, huku nchini Uholanzi nayo imeanza kufunga baadhin ya maeneo kama mikahawa.