KAMPALA,UGANDA

KAMPUNI ya kuchimba mafuta ya Tullow imepata ruhusa kutoka Serikali ya Uganda,kuuza mgao wake wa machimbo ya mafuta katika eneo la ziwa Albert kwa kampuni ya Ufaransa ya total.

Hatua hiyo inatarajia kutoa fursa ya kuanza kwa hatua ya mwisho ya uwekezaji katika kuchimba na kusafirisha mafuta ya Uganda kwa soko la kimataifa,ikiwemo ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta hayo kutoka Hoima Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, kampuni ya Tullow ilisema kwamba Serikali ya Uganda na mamlaka ya kukusanya ushuru Uganda  URA, zilifikia makubaliano kuhusu namna ya kulipa ushuru kutokana na kuuza kwa vifaa vyake kwa kampuni ya Total.

“Waziri wa nishati na maendeleo ya madini wa Uganda aliidhinisha hatua ya kupeana vifaa na mali za Tullow kwa kampuni ya Total pamoja na idhini ya utendaji kazi katika machimbo namba mbili,”ilisema taarifa ya Tullow.

Kampuni ya Tullow itapokea dola milioni 500 katika hatua ya kwanza na dola milioni 75 maamuzi ya uwekezaji ya mwisho yatakapochukuliwa kuhusu mradi huo wa kuchimba mafuta.

Kampuni ya Tullow pia ina haki ya kupokea sehemu ya pesa zitakazopatikana katika awamu ya kwanza ya uchimbaji mafuta hayo.

Tangu mwaka 2016, Uganda imekuwa ikikumbana na changamoto kadhaa za kisheria, kuhusiana na uchimbaji mafuta yake yanayotarajiwa kuelea dola bilioni 3.5.

Mnamo mwaka 2019 mradi huo wa kuchimba mafuta ulikumbana na changamoto kubwa baada ya kampuni ya Total kujiondoa katika mradi

wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta, kufuatia hatua ya kuvunjika kwa mkataba wa kununua sehemu ya mali za kampuni ya mafuta ya Tullow kwenye mradi wa maendeleo wa Albert.

Kampuni ya Total ilikubali kununua mali za Tullow nchini Uganda kwa gharama ya dola milioni 575, katika hatua iliomaliza mzozo wa ushuru na Serikali.

Katika makubaliano ya sasa, Kampuni ya Total itamiliki asilimia 33.33 katika kila leseni ya kuchimba mafuta katika ziwa Albert, pamoja na mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta hayo.