MADRID,UHISPANIA

UHISPANIA imetangaza hali ya kitaifa ya dharura ili kupambana na wimbi la pili la virusi vya corona.

Wakati ugonjwa huo ukiendelea kuenea kwa kasi Ulaya, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez pia alitangaza amri ya kutotembea nje usiku kote nchini humo isipokuwa katika Visiwa vya Canary.

Italia ambayo ilikuwa kitovu cha mripuko wa kwanza Ulaya pia iliimarisha vizuizi vya maisha ya kila siku,kwa kuamuru kufungwa kumbi za sinema na mazoezi pamoja na mabaa na migahawa.

Waandamanaji kadhaa wa misimamo mikali mjini Rome walikabiliana na polisi ya kuzuia ghasia usiku kucha wakati wa maandamano ya kupinga amri ya kutotembea nje.

Polisi mjini Berlin pia waliyavunja maandamano ya kupinga vizuizi vya corona, na kuanzisha uchunguzi baada ya jengo lenye ofisi za shirika la afya ya umma kushambuliwa kwa moto.