BERLIN,UJERUMANI

UJERUMANI na Ufaransa zimependekeza Umoja wa Ulaya uiwekee vikwazo Urusi kutokana na kuhusika kwake kumuwekea sumu kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa nchi hizo mbili zinataka vikwazo hivyo viwalenge watu binafsi wanaodaiwa kuhusika na uhalifu huo na kukiuka sheria za kimataifa, pamoja na taasisi iliyohusika na mpango wa sumu ya Novichok.

Shirika la Kimataifa la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali, OPCW lilithibitisha kwamba Navalny alipewa sumu ya Novichok inayoharibu mishipa ya fahamu.

Aidha, taarifa kutoka Uingereza, zinaeleza kuwa nchi hiyo inaunga mkono mpango wa mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas na wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian wa kuiwekea Urusi vikwazo.

Hata hivyo, Urusi imeyakanusha madai hayo.