MNAMO Oktoba 16 mwalimu mmoja aliyetambulika kwa jina la Samuel Paty alikatwa kichwa nchini Ufaransa, kufuatia hatua yake ya kuwaonesha wanafunzi katuni ya Mutume Muhammad (SAW).

Tukio hilo kukatwa kichwa kwa mwalimu huyo liliripotiwa kutokea katika kiunga cha Conflans Saint-Honorine kilicho umbali wa kilomita 30 kutoka katikati ya mji mkuu, Paris, majira ya saa 11:00 jioni, karibu na skuli anayofundisha mwalimu huyo.

Ripoti zinaeleza kwamba, mwalimu huyo wa somo la historia, alikuwa amewaonesha wanafunzi wake picha, zenye katuni za Mtume Muhammad (S.A.W), ambapo kabla ya kuonesha picha hizo aliwaomba wanafunzi wa kiislamu watoke nje ya darasa ili asiwaumize kihisia.

Suala la kuoneshwa picha ama katuni za Mtume nchini Ufaransa limekuwa likifanyika sana nchini humo kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni, hata hivyo matukio ya kuonesha katuni ama picha za kiongozi huyo wa dini ya kiislamu, yanachukuliwa na waislamu kama kufuru.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye alilitembelea eneo la tukio, alisema taifa zima linaungana pamoja dhidi ya kile alichokiita mashambulizi ya kigaidi.

Aidha Macron aliapa kupambana dhidi ya kile alichokiita kujitenga kwa wafuasi wa itikadi kali ya uislamu, ambapo alisema kunatishia kuchukua udhibiti wa baadhi ya jamii za waislamu nchini Ufaransa.

Kilichoukasirisha ulimwengu wa kiislamu ni hatua ya kauli ya rais huyo aliyesema kuwa Ufaransa haitoacha kuchora vibonzo, kutokana na kuchinjwa kwa mwalimu Samuel Paty.

Kauli huyo ya rais Macron ikiwafanya wale wanaouchukia uislamu wachapishe zaidi vibonzo hivyo vya kufuru ambapo ripoti zinaeleza kuwa vilibandikwa kwenye majengo ya serikali nchini Ufaransa, hatua ilizidu kuukasirisha ulimengu wa kiislamu.

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alimshambulia Macron akisema kiongozi huyo anahitaji matibabu ya akili kutokana na mtazamo wake kwa waislamu na uislamu.

“Ni nini tatizo la huyu mtu anaeitwa Macron na uislamu na waislamu? Macron anahitaji matibabu ya akili,” Erdogan alisema katika hotuba aliyoitoa wakati mbele ya wafuasi wake wa chama cha AKP katika mji wa katikati mwa Uturuki wa Kayseri.

“Nini kingine kinaweza kusemwa kwa mkuu wa nchi asieelewa uhuru wa imani na mwenye tabia ya namna hii kwa mamilioni ya watu wanaoishi nchini mwake, ambao ni waumini wa dini tofauti?” Erdogan aliongeza.

Erdogan ni muislamu na tangu chama chake cha AKP chenye misingi ya kiislamu kiingie madarakani mwaka 2002, ameufanya uislamu kuwa sehemu ya siasa nchini Uturuki, taifa lenye idadi kubwa sana ya waislamu, lakini linafuata misingi ya kilimwengu.

Rais Erdogan alitoa wito kwa Waturuki kususia bidhaa kutoka Ufaransa, “Kama vile huko Ufaransa wengine wanasema” usinunue bidhaa kutoka Uturuki “, hapa ninalihutubia taifa: ninawaomba, msusie bidhaa kutoka Ufaransa, msinunue,” alisema Erdogan.

“Kampeni ya kuua watu kwa mawe sawa na ile dhidi ya Wayahudi wa Ulaya kabla ya vita ya pili ya dunia inaendeshwa dhidi ya waislamu”,aliongeza rais huyo.

Ufaransa imeijibu kauli hiyo kwa kumuita balozi wake aliyeko Ankara na imeikosoa propaganda ya Uturuki ikisema inalenga kuchochea chuki nyumbani na nje ya nchi.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ameyaita matamshi ya Erdogan kuwa yasiyokubalika’ na ameitaka Uturuki kuacha uhasama huo hatari wa kujibizana.

Hivi sasa wito wa kususia bidhaa za Ufaransa unavuma kwenye mitandao ya kijamii, huku wananchi wa Misri wakisambaza orodha ya bidhaa za kifaransa walizoamua kuzisusia.

Imam mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Al-Azhar mjini Cairo, Ahmed al-Tayyeb alisema shambulizi dhidi ya Mtume Muhammad ni sehemu ya kampeni ya kuutumia uislamu kushinda vita vya kisiasa.

Nchini Kuwait, mashirika 50 ya ushirikiano wa kibiashara yamesema yameondoa bidhaa zote za Ufaransa katika maduka yake kwenye nchi hiyo ya Ghuba, ambapo pia hatua kama hiyo imeripotiwa kuchukuliwa nchini Qatar.

Jumuia ya nchi za kiislamu, (OIC) imelaani kitendo cha kuchora vibonzo vinavyomuonesha kiongozi huyo wa dini ya kiislamu, ikisema ni ”hatari kwa uhusiano” wa nchi za kiislamu na Ufaransa.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Jordan, pia ameikosoa hatua ya Ufaransa iliyotumika kwa kisingizo cha uhuru wa kujieleza.

Wizara ya mambo ya nje ya Morocco imelaani vikali hatua ya kuendelea kuchapishwa vibonzo hivyo, ikisema uhuru wa kujieleza hauwezi kuhalalisha kuitukana dini ya kiislamu, ambayo ina zaidi ya waumini bilioni mbili ulimwenguni kote.

Ufaransa imeukosoa wito wa kususiwa kwa bidhaa zake, ikitaka hatua hiyo ikomeshwe na kusema kwamba mashambulizi kama hayo ni kazi ya waislamu wachache wenye itikadi kali na kusisitiza kuhusu msimamo uliotolewa na Rais Macron kwamba Ufaransa haitopiga marufuku uchapishaji wa vibonzo hivyo.

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imemuita balozi wa Ufaransa nchini humo kulalamika kuhusu kitendo cha Rais Macron kuunga mkono kuchapishwa vibonzo vya Mtume Muhammad.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Shah Mehmood Qureshi amesema kuwa matendo kama hayo yanachochea chuki na kuigawa jamii na inaweza kusababisha tatizo kubwa duniani.