ABUJA,NIGERIA

NCHI  ya Nigeria inaendelea kukumbwa na hali ya machafuko baada ya askari usalama kuwatawanya kikatili vijana walioandamana dhidi ya ghasia za polisi, na kuua watu kadhaa.

hayo yalitangazwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.

Ripoti zinasema kuwa, wakaazi wengi walilazimika kujifungia majumbani mwao huko Lagos, Jiji  na jimbo  lenye watu milioni 20 ambapo sheria ya kutotoka nje, iliyotangazwa, iliongezwa muda hadi saa 72.

Visa vya uporaji na uharibifu mkubwa viliripotiwa katika maeneo kadhaa ya Jiji la Lagos, na barabara nyingi zilikuwa na vizuizi vilivyowekwa na makundi ya watu waliokuwa na hasira.

Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat alilaani vurugu zinazoendelea nchini Nigeria.

Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kukomeshwa ukatili wa polisi nchini Nigeria, nchi ambayo imekumbwa na maandamano kwa wiki mbili sasa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema katika taarifa kuwa Guterres alivihimiza vikosi vya usalama vya Nigeria kujiuzia na aliwataka raia kufanya maandamano kwa amani na kujiepusha na machafuko.

Maandamano zaidi yalishuhudiwa kote nchini Nigeria kupinga mienendo ya kikosi maalumu cha polisi wa kukabiliana na wizi (SARS) kinacholaumiwa kwa kuendesha vitendo vya kikatili nchini humo.