OTTAWA, CANADA

JUMLA ya nchi 168 zimejiunga na mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuandaa chanjo ya maradhi ya Covid-19 huku Uingereza,Canada na Ujerumani zikiahidi kutoa karibu dola bilioni moja kuchangia mpango huo.

Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyengine tena aliomba msaada kwa nchi za dunia ili kupata chanjo ya kudhibiti maradhi ya Covid-19. 

Uingereza,Canada,Ujerumani na Sweden ziliahidi kutoa msaada wa fedha wa karibu dola bilioni moja ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kupata chanjo ya Covid-19 na matibabu yake.

Mpango huo wa Umoja wa Mataifa unaoongozwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), na muungano wa chanjo wa GAVI hadi sasa ulipokea dola bilioni tatu lakini dola bilioni 35 nyengine zinahitajika katika uwanja huo.

Mpango huo wa kutafuta chanjo ya kukabiliana na maradhi ya Covid-19 una lengo la kutoa dozi bilioni mbili hadi kufikia mwishoni mwa mwaka ujao,kutoa matibabu milioni 245 na kupima wagonjwa milioni 500.

Akizungumza wiki hii katika kikao cha ngazi ya juu kuhusu mpango huo, Antonio Guterres alisema ni kwa maslahi ya kitaifa na kiuchumi ya kila nchi kufanya kazi pamoja ili wananchi waweze kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu na vile vile kupatikana chanjo hiyo kwa bei nafuu.