KINSHASA,CONGO

UJUMBE wa Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa uliohudumu kwa zaidi ya miongo miwili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huenda ukapunguzwa katika maeneo kadhaa kwa kipindi cha miaka michache ijayo.

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres iliyochapishwa wiki hii na kuonyeshwa shirika la habari la AFP inaeleza mbinu ambazo ujumbe huo unaweza kupunguzwa bila kuweka muda wa mwisho wa kujiondoa kabisa nchini humo.

Ujumbe wa kulinda amani unaofahamika kama MONUSCO umekuwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa zaidi ya miaka 20 ukiwa na bajeti ya kila mwaka ya karibu dola bilioni moja na karibu askari 15,000.

Guterres alisema ujumbe huo utaimarisha uwepo wake katika mikoa mitatu inayoendelea kushuhudia migogoro ambayo ni Kivu Kaskazini na Kusini, iliyoko mashariki mwa nchi, na Ituri katika upande wa kaskazini mashariki.

Guterres alisema serikali ilikubali kuwa wanajeshi wa ujumbe huo waondoke katika mkoa wa Kasai kufikia Juni 2021, na mkoa wa kusini mashariki wa Tanganyika mnamo 2022.