KINSHASA,CONGO

MIAKA kumi iliyopita, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ilichapisha ripoti yake kuhusu utelekezaji wa haki za binadamu huko Congo DR.

Ripoti hiyo ilijumuisha vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa vilivyofanywa nchini humo kati ya Machi 1993 na Juni mwaka 2003.

Uchunguzi wa aina hiyo ambao haujawahi kufanywa ulikusudia kukomesha jinai hizo zilizoendelea kwa zaidi ya muongo mmoja katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa, wananchi wa Congo zaidi ya milioni nne walipoteza maisha ikiwa ni matokeo ya moja kwa moja au  yasiyo ya moja kwa moja ya mizozo iliyoikumba nchi hiyo huku mabinti na wanawake zaidi ya 40,000 wakitumiwa kama watumwa wa ngono, na watu wengine milioni tatu wakilazimika kuwa wakimbizi.

Licha ya kutolewa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, lakini hakuna jinai yoyote kati ya hizi iliyofunguliwa mashitaka,suala ambalo limelaumiwa na kukosolewa pakubwa na wananchi wa Congo.

Mmoja ya wakosoaji wa jinai hizo ni Dr. Denis Mukwege mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ilitaja vitendo 617 vya ukatili na utumiaji mabavu vilivyofanyika katika mikoa yote ya nchi hiyo na kutaja nafasi ya makundi ya congo na ya nchi ajinabi katika kutenda jinai hizo yakiwemo majeshi au makundi yenye silaha kutoka Rwanda, Uganda, Burundi na Angola.

Zoezi hilo la kuhakiki ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa nchini Congo lililofanyika miaka kumi iliyopita kwa usaidizi wa serikali ya Congo.

Hata hivyo Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa, mfumo wa sheria wa nchi hiyo hauna uwezo wala dhamana ya kutosha ya kuhakikisha kuwa haki inatendeka na wahusika wa jinai hizo wanachukuliwa hatua.