NA MWANTANGA AME

JANA ni siku ya kunawa mikono kimataifa ambapo dunia inaadhimisha siku hiyo ikiwa ni sehemu ya kuikumbusha jamii juu ya suala zima la usafi huo.

Hii ni kutokana na kwamba wengi wanajamii kuonekana suala hili kama sio la lazima, na hauna maana yoyote kwani wapo wanaothubutu hata kula bila ya kunawa mikono ama kunyonyesha watoto.

Leo hii, imeonekana suala la kunawa mikono kuwa ni moja ya kero kubwa kwa jamii kiasi ambacho baadhi ya mashirika ya kimataifa kufadhili aina ya matangazo yanayohimiza usafi wa kunawa mikono.

Suala hili limekuwa ni gumu kutekelezeka kutokana na baadhi ya wenye tabia hii hawaonekani kujali afya zao kwa vile wanaona wasipo fanya wayatakayo, kisa kunawa mikono huwa hawafikwi na maradhi yoyote.

Ushahidi wa hilo hivi karibuni yalipoanza maradhi ya Covid 19, ama Corona, ambapo sehemu ya kinga yake iliwataka wananchi wote kuwa na tabia ya kunawa mikono kila wakati.

Tabia hiyo, ilionekana kuwa ni kikwazo kwa baadhi ya wananchi, kwani walithubutu kutotii sharti hilo pale zilipowekwa huduma hizo kila ofisi za serikali na za kijamii kiasi ambacho ilionesha wazi kuwa tabia ya hiyo haikuwa ni mazoea yao.

Baya zaidi ambalo lilijionesha katika sehemu hizo pale huduma ya maji yanayowekwa kumalizika, basi wasimamizi walikuwa hawajali kuyajaza tena ili watu waendelee kupata huduma hiyo.

Kuna baadhi ya maeneo yalionekana kuwekwa huduma hiyo ya kuosha mikono ikitumiwa kinyume chake kwani wapo waliotumia maji hayo kuoshea vyombo badala ya kunawa mikono, jambo ambalo linaonesha kutokuwepo kwa umakini katika hilo.

Hili limeonekana zaidi pale tuu zilipotoka taarifa za kumalizika kwa ugonjwa huo, kwani kila sehemu zilizwekwa ndoo ya maji na sabuni zimeondolewa na hata ile dawa za sanitize nazo hazipo tena, jambo ambalo linadhihirisha tabia hiyo kama imewachosha watu na wala hawana haja nayo kwani sio utamaduni wao.

Hiyo ni kutokana na kwamba wengi wanajamii wamekuwa wanauchukia utamaduni huu kiasi ambacho mazoweya yake kuwa ni ya tabu kuufuata licha ya kuwa ni usalama kwa afya zao.