KINSHASA, DRC

MFUKO wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF)umetangaza kuwa,unaendelea kutiwa hofu kubwa kuhusu maelfu ya watoto walio hatarini wakati machafuko yakiendelea kwenye jimbo la Ituri lililoko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo watoto wanaendelea kuteseka kwa sababu ya machafuko na vurugu zilizosababishwa na vita vya muda mrefu katika jimbo hilo.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) unasema kuwa, machafuko yalishika kasi mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020 na tangu wakati huo hali kwa maelfu ya watoto jimboni Ituri imezidi kuzorota.

Mashambulizi ya wanamgambo katika maeneo ya raia yalisababisha mamia ya vifo na UNICEF ilipokea taarifa za watoto kujeruhiwa,kuawa au kuingizwa kwenye mapigano na makundi yenye silaha na kutumiwa kama askari vitani.

Wakati huohuo zaidi ya watu milioni 1.6 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wanakadiriwa kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mchafuko hayo.

Kwa mujibu wa UNICEF kati ya Januari na Juni mwaka huu,watoto wasiopunguua 91 waliuawa, 27 kujeruhiwa na 13 ni waathirika wa ukatili wa kingono.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maofisa usalama kwa upande mwengine,kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.