NEW DELHI,INDIA

SHIRIKA la kimataifa linaloshughulikia masuala ya watoto na wasichana, Plan International limesema unyanyasaji wa mitandaoni umesababisha wasichana kuacha kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Hayo ni kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa na shirika hilo ambao uliwajumuisha wasichana 14,000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 25 kwenye nchi 22, ikiwemo Brazil, Benin, Marekani na India.

Utafiti huo ulisema zaidi ya wasichana asilimia 58 walikumbana na unyanyasaji wa mitandaoni.

Mtendaji Mkuu wa Plan International, Anne-Birgitte Albrectsen alisema wasichana wananyamazishwa kwa kunyanyaswa vibaya mitandaoni.

Asilimia 39 ya wasichana walikumbana na unyanyasaji kwenye mtandao wa Facebook, asilimia 23 Instagram, asilimia 14 Whatsapp, asilimia kumi Snapchat, asilimia tisa Twitter na asilimia sita Tiktok.

Unyanyasaji mkubwa waliokumbana nao wasichana hao ni pamoja na lugha za matusi, kuchekwa maumbile yao pamoja na vitisho vya unyanyasaji wa kijinsia.