Dk. Magufuli 80%, Dk. Mwinyi 67%

Vigezo vya ushindi vyabainishwa

NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa na kampuni ya Trends Dynamiques Consulting ya jijini Nairobi nchini Kenya, umebainisha kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. John Pombe Magufuli ataongoza kwa asilimia 79.

Utafiti pia umebainisha kuwa mgombea wa urais wa Tanzania kupitia Chama cha CHADEMA, Tundu Lissu atapata asilimia 19 na wagombea wa vyama vyengine watapata asilimia mbili katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Kwa upande wa Zanzibar mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Hassan Mwinyi atachaguliwa kwa asilimia 67 dhidi ya mgombea wa Chama cha ACT – Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad atakayeibuka na asilimia 30 na wagombea wa vyama vyengine wataambulia asilimia tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa kampuni ya Trends Dynamiques Consulting ya Nairobi, Mulubi Asiligwa, alisema utafiti huo umewashirikisha watoa maoni ya uchaguzi.

Alifahamisha kuwa utafiti ulianza kufanywa mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu, ambao uliwahusisha vijana na wazee kuanzia umri wa miaka 18 hadi 66, wanaume na wanawake.

Alisema jumla ya wapiga kura 9,716 walitoa maoni hayo, ambapo kwa Tanzania bara walikuwa 7,397 na Zanzibar walikuwa 2,319, kwa kuwajumuisha wanaume asilimia 44 na wanawake asilimia 56 kwa mikoa yote 26 ya Tanzania.

Aliongeza kusema kwamba, Dk. Magufuli (CCM), kwa upande wa kura zitazopigwa Tanzania bara atashinda kwa asilimia 80, huku Lissu wa CHADEMA atapata asilimia 18 na wagombea wa vyama vyengine watapata asilimia mbili, kati ya watoa maoni asilimia 94 wataopiga kura mwaka huu.

Alieleza kwa upande wa visiwa vya Zanzibar, mgombea urais wa Tanzania (CCM), Dk. Magufuli atashinda kwa asilimia 71, mgombea urais (CHADEMA) Lissu atapata asilimia 28 na vyama vyengine asilimia moja.

Alisema kuchaguliwa kwa Dk. Magufuli kunatokana na sababu mbali mbali ikiwemo sio mla rushwa, uwezo wa kulinda maslahi ya taifa, ujenzi wa miundombinu, uadilifu, uchapakazi, usimamizi wa miradi, ubora wa ilani ya CCM na uwezo wake wa kulinda maslahi ya taifa.

Aidha alifafanua kuwa, kwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi ataongoza kwa kura katika visiwa hivyo kwa asilimia 67, ambapo mgombea urais wa ACT- Wazalendo Maalim Seif Sharifu Hamad atapata kura asilimia 30 na vyama vyengine asilimia tatu. 

Alisema Dk. Mwinyi kashinda kwa asilimia 67 baada ya wapiga kura asilimia 96 kuthibitisha hilo kwa kusema sio mla rushwa, muadilifu katika kusimamia maslahi ya Zanzibar na muungano, ana maamuzi stahili na ilani ya chama chake ipo vizuri.

Akijibu maswali ya waandishi, alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) licha ya kuwa kikongwe lakini kimeendelea kuzoa umaarufu na kupendwa zaidi kikifuatiwa na cha CHADEMA kwa umbali sana.