NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya Wilaya Mwanakwerekwe imemhukumu Mohammed Sleyum Salum (37) mkaazi wa Kijichi Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa siku 120.

Hakimu Asya Abdalla Ali, wa mahakama hiyo alitoa hukumu hiyo kwa mshitakiwa huyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo dhidi ya shitaka lilokuwa likimkabili la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Asya, alisema mahakama inamuona mshitakiwa huyo kuwa ni mkosa na kumtaka kulipa faini ya shilingi 500,000 au kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa siku 120.

Mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo na kupelekwa Chuo cha Mafunzo kutumikia adhabu yake aliyopewa mahakamani hapo.

Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Nassra Khamis alidai, kuwa kesi hiyo ipo kwa ajili ya kutolewa hukumu kwani upande wa mashitaka umeshawasilisha mashahidi sita na mshitakiwa huyo ameshajitetea mahakamani hapo.

Ilidaiwa kuwa mnamo mwaka 2017 nyakati tofauti huko Bububu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mshitakiwa huyo aliaminiwa kwa kupewa shilingi 7,000,000 kwa lengo la kuzipeleka benki ya SACCOS ambapo alishindwa kuzipeleka Benki na wala kuwarejeshea wanakikundi cha Mkorofi si Mwenzetu.

Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Julai 17 na hukumu ilitolewa Oktoba 1, mwaka huu.